Inachokifanya Barcelona ni kama Yanga
Muktasari:
- Usajili huu ukikamilika unadaiwa utakuwa ni wakwanza kwa takriban miongo mitatu sasa tangu mchezaji wa mwisho afanye uhamisho wa moja kwa moja kutoka Real Madrid kwenda Barcelona.
BARCELONA, HISPANIA: WAKATI Tanzania Yanga ikidaiwa kufikia makubaliano ya kumsajili Mohame Hussein Tshabalala kutoka kwa majirani zao Simba, kule Hispania mambo pia yapo hivi baada ya Barcelona kuripotiwa inataka kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Mbrazil Rodrygo katika dirisha hili na tayari imeshawasiliana na wawakilishi wake kwa ajili ya kukamilisha dili hilo.
Usajili huu ukikamilika unadaiwa utakuwa ni wakwanza kwa takriban miongo mitatu sasa tangu mchezaji wa mwisho afanye uhamisho wa moja kwa moja kutoka Real Madrid kwenda Barcelona.
Katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka 1996, Luis Enrique aliacha mkataba wake umalizike akiwa Santiago Bernabeu ili ajiunge na Barcelona kama mchezaji huru jambo lililowaudhi sana mashabiki wengi wa Madrid.
Baadaye alieleza, alijisikia kutothaminiwa na mashabiki wa Madrid na hana kumbukumbu nzuri alipokuwa huko, licha ya kucheza mechi zaidi ya 150 katika kipindi cha miaka mitano jijini humo.
Tangu uhamisho huo, hakuna mchezaji aliyethubutu kufuata nyayo za Enrique lakini hilo linaweza kubadilika dirisha hili baada ya Barcelona kuanza harakati za kumshusha Rodrygo Camp Nou.
Ripoti kutoka tovuti ya UOL Esporte ya Brazil inadai Barcelona wanaufuatilia kwa karibu mustakabali wa Rodrygo na sasa klabu hiyo ya Catalonia ipo katika mazungumzo na wawakilishi wake.
Hakuna muafaka wowote uliofikiwa kwa sasa, kwa mujibu wa ripoti hiyo, lakini mabingwa hao watetezi wa La Liga wameweka wazi wako tayari kujadiliana iwapo Rodrygo atakuwa tayari kujiunga nao.
Habari hii imeibuka wakati Barcelona pia inaendelea na mpango wa kumsajili mshambuliaji wa Manchester United, Marcus Rashford kwa mkopo wenye kipengele cha kumnunua kabisa katika dirisha hili.