Ile penalti ya Atletico ni hivi

Muktasari:
- Katika mchezo huo ambao Madrid ilifanikiwa kupita kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Kylian Mbappe, Jude Bellingham pamoja na Alexander Sorloth kwa upande wa Atletico walifunga penati tatu za mwanzo kwa ustadi mkubwa huku Alvarez akionekana kufuata njia hiyo, akikwamisha mpira wavuni lakini katika hali iliyoshangaza wengi penalti ilikataliwa.
MADRID, HISPANIA: MOJA kati ya matukio yaliyojiri katika usiku wa michuano ya Ligi ya Mabingwa juzi ilikuwa ni kukataliwa kwa penalti ya staa wa Atletico Madrid Julian Alvarez tukio ambalo lilishangaza watu wengi.
Katika mchezo huo ambao Madrid ilifanikiwa kupita kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 4-2 baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Kylian Mbappe, Jude Bellingham pamoja na Alexander Sorloth kwa upande wa Atletico walifunga penati tatu za mwanzo kwa ustadi mkubwa huku Alvarez akionekana kufuata njia hiyo, akikwamisha mpira wavuni lakini katika hali iliyoshangaza wengi penalti ilikataliwa.
Moja ya sababu zinaelezwa kusababisha penalti hiyo kukataliwa ni kwamba nyota huyo wa zamani wa Manchester City aliteleza alipochukua mpira. Ingawa awali ilikubalika, tukio hilo lilikaguliwa kwa haraka kupitia VAR na baadae ikakataliwa.
Alvarez alihukumiwa kwa kugusa mpira mara mbili, akianza kwa mguu wake wa kushoto alipoteleza na kisha kwa mguu wake wa kulia alipopiga shuti lake.
Kitendo hicho kililalamikiwa na wachezaji wa Madrid na kwa mujibu wa kanuni za FIFA zinasema penalti lazima ipigwe kwa kugusa mpira mara moja, hivyo shuti la Alvarez halikuwa halali kwa sababu alifanya zaidi.
Penalti yake ilikataliwa na mikwaju ya penati ikaendelea. Maelfu ya mashabiki wa Atletico waliokuwa uwanjani hawakujua kuwa penalty ya Alvarez ilikuwa imekataliwa na walidhani mikwaju ya penati ilikuwa bado sawa. Antonio Rudiger alisimama na kufunga penalti ambayo iliipeleka Madrid hadi robo fainali.
Kipa wa Madrid Thibaut Courtois alikuwa miongoni mwa wale waliokuwa na uhakika kwamba Alvarez alikuwa amegusa mpira mara mbili, na mara moja alimjulisha mwamuzi Szymon Marciniak.
“Nilihisi kuwa Julan aligusa mpira mara mbili na nikamwambia mwamuzi,” alisema Courtois.
“Walikuwa na bahati mbaya kidogo. Hatukucheza vizuri leo, lakini tumeshinda, na hiyo ndiyo muhimu.”
Kocha wa Atletico, Diego Simeone alionekana kuwa ni mwenye hasira na kuchukizwa kwa kitendo hicho akiamini mchezaji wake hakuwa amegusa mpira.
"Wote tulikuwa pale nani aniambie kwamba Alvarez aligusa mpira mara mbili anyooshe mkono. Hii ni mara yangu ya kwanza kushuhudia penalti inaangalia kwenye VAR,"alisema kocha huyo katika mkutano wake na waandishi wa habari.