Ibrahimovic kuzeekea Milan

Muktasari:

STAA wa AC Milan na timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic anatarajia kusaini mkataba mpya utakaomfanya kucheza kwenye viunga hivyo kwa mwaka mmoja zaidi hadi atakapofisha umri wa miaka 40.

MILAN, ITALIA

STAA wa AC Milan na timu ya taifa ya Sweden, Zlatan Ibrahimovic anatarajia kusaini mkataba mpya utakaomfanya kucheza kwenye viunga hivyo kwa mwaka mmoja zaidi hadi atakapofisha umri wa miaka 40.
Ibrahimovic anatarajia kufikisha umri huo ifikapo Oktoba 03, mwaka huu lakini hadi sasa hajaonyesha kushuka kiwango licha ya umri kumtupa mkono.
Kwenye Seria A msimu huu ameshafunga mabao 15 katika mechi 16 za michuano yote alizocheza na kuiwezesha timu hiyo kushika nafasi ya pili nyuma ya Inter Milan.
Taarifa kutoka  Sky Sports Italy, zimefichua kwamba baada ya uvumi uliokuwa una sambaa juu ya jamaa kuondoka mwisho wa msimu huu, viongozi wa Milan wamekaa naye na kufikia makubaliano ya kumuongeza mkataba wa mwaka mmoja.
Vilevile Sky imeeleza kuwa dili hilo anatarajia kusaini ndani ya siku 10 zijazo kuanzia sasa.
Hata hivyo, hakutakuwa na mabadiliko ya mshahara anaoupokea sasa wa Pauni 5.49 milioni kwa mwaka.
Wachezaji wengine ambao Milan inatarajia kuwaongeza mikataba na mazungumzo bado yanaendelea ni golikipa wao namba moja Gianluigi Donnarumma na kiungo kutoka Uturuki,  Hakan Calhanoglu.
Ibrahimovic alijiunga na AC Milan mwaka 2020 baada ya kukiwasha akiwasha akiwa na LA Galaxy na  Manchester United.