Huyu Ronaldo kashindikana

Tuesday January 12 2021
ronaldo pic

Turin, ITALIA. BAO la ushindi la dakika za majeruhi alilofunga dhidi ya Sassuolo juzi, lilimwezesha nyota wa Juventus, Cristiano Ronaldo kuifikia rekodi ya upachikaji mabao ya Josef Bican ya ufungaji wa muda wote katika historia ya soka.

Baada ya kupachika bao hilo, Ronaldo sasa ameifikia rekodi ya ufungaji ya Bican aliyefumania nyavu mara 759 katika ngazi ya klabu na timu ya taifa ambayo ilidumu kwa muda wa miaka 66.

Bican alitumia muda wa miaka 24 kuanzia mwaka 1931 hadi 1955 alipochezea timu ya taifa ya Czech na klabu za Rapid Vienna, Admira, Slavia Plague, FC Vitkovice, FC Hradec Kralove na Dynamo Plague.

Lakini Ronaldo yeye ametumia muda wa miaka 19 tu kuifikia na pengine kuja kuivuka akichezea timu ya Taifa ya Ureno na klabu za Sporting, Manchester United, Real Madrid na sasa Juventus. Idadi kubwa ya mabao kati ya hayo 759 ambayo Ronaldo amefumania, ameyafunga akiwa na kikosi cha Real Madrid ikifuatiwa na Manchester United, pia na timu ya taifa ya Ureno.

Nyota huyo wa Ureno ameifungia Real Madrid jumla ya mabao 450 katika mechi 438 alizoichezea wakati Manchester United ameifungia jumla ya mabao 118 katika idadi ya mechi 292 alizokuwa kikosini kabla ya kuuzwa mwaka 2009.

Timu ya Taifa ya Ureno ameifungia jumla ya mabao 102, mabao 86 akiyafunga katika mechi 108 za Juventus huku Sporting Lisbon akiifungia jumla ya mabao matano katika idadi ya mechi 31.

Advertisement

Kabla ya bao hilo, Ronaldo alikuwa akishika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu akiwa amepachika jumla ya mabao 758 akiwapiku ‘Mfalme wa Soka’ duniani, Pele pamoja na hasimu wake mkubwa kwa sasa, Lionel Messi.

Mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni aliibuka mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa karne wa tuzo za Soka za Globe, sasa anahitaji kufunga bao moja tu ili rasmi awe mfungaji bora wa muda wote hapa duniani.

Katika mchezo huo ambao Juventus waliibuka na ushindi wa mabao 3-1, Danilo alianza kuifungia bao la kuongoza Juventus katika dakika ya 50 lakini dakika nane baadaye lilisawazishwa na Gregoire Defrei.

Aaron Ramsey aliwarudisha tena mchezoni Juventus baada ya kuwafungia bao la pili katika dakika ya 82 kisha Ronaldo akaja kufunga hesabu dakika za majeruhi na kuihakikishia ushindi timu yake ambao uliisogeza hadi nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Italia.

Bao hilo lilitokana na pasi ndefu ya Danilo ambayo ilitulizwa vyema na Ronaldo ambaye aliujaza wavuni kwa shuti la mguu wa kulia lililomshinda kipa wa Sassuolo, Andrea Consiggli.

Ni mechi iliyotawaliwa na Juventus kwa kiasi kikubwa huku ikishuhudiwa jumla ya kadi sita zikitolewa miongoni mwa hizo ikiwa ni nyekundu iliyoonyeshwa kwa mshambuliaji wa Sassuolo, Pedro Obiang kutokana na rafu aliyocheza kwa Federico Chiesa.

Advertisement