Haya Zirkzee asema kitu kuhusu Musiala

Muktasari:
- Joshua Zirkzee, ambaye aliwahi kucheza na kiungo Musiala huko Bayern Munich, kabla ya kuhamia zake Bologna, amefichua namna anavyojaribu kumshawishi Mjerumani huyo ili wakakipige pamoja huko Old Trafford.
MANCHESTER, ENGLAND: MASHABIKI wa Manchester United wanakoshwa na taarifa za kuwapo uwezekano wa kumsajili Jamal Musiala baada ya staa wao mpya kuzungumzia jambo hilo.
Joshua Zirkzee, ambaye aliwahi kucheza na kiungo Musiala huko Bayern Munich, kabla ya kuhamia zake Bologna, amefichua namna anavyojaribu kumshawishi Mjerumani huyo ili wakakipige pamoja huko Old Trafford.
Zirkzee alijiunga na Man United kwa ada ya uhamisho wa Pauni 34 milioni kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi huko Ulaya akitokea kwa miamba hiyo ya Serie A. Na alisema anajaribu kumshawishi Musiala atue kukipiga Old Trafford.
Shabiki mmoja alimuuliza Zirkzee kama amejaribu kumshawishi Musiala ajiunge Man United, alijibu: “Nimejaribu, nilijaribu.”
Mashabiki walimwona Kobbie Mainoo akizungumza na Zirkzee kuhusu kujiunga na Man United wakati England ilipocheza na Uholanzi kwenye Euro 2o24 huko Ujerumani. Wawili hao walionekana wakizungumza baada ya mechi kumalizika na siku chache baadaye, Zirkzee alisaini miaka mitano Man United. Na kwenye hilo, Mdachi Zirkzee alisema: “Kobbie aliniuliza kama nakuja. Nilimwambia tutaonana baada ya fainali hizi.” Musiala amekuwa akihusishwa na Manchester City kwenye dirisha hili.
Staa huyo mwenye umri wa miaka 21 alifanya vizuri kwenye Euro 2024 na aliifungia Ujerumani mabao mawili kabla ya kukwama kwenye hatua ya robo fainali ilipochapwa na Hispania.