Napoli yajipanga kumng’oa Jack Grealish Etihad

Muktasari:
- Ripoti za kutoka England zinafichua vinara hao wa Serie A, Napoli wanamfukuzia kwa karibu supastaa huyo wa Manchester City, aliyenunuliwa kwa pesa nyingi Pauni 100 milioni, ili kwenda kucheza kwenye timu yao kuanzia msimu ujao.
JACK Grealish anaripotiwa kuwa na mpango wa kuachana na Ligi Kuu England mwishoni mwa msimu huu ili akakipige Serie A baada ya miamba ya Italia, Napoli kuhitaji saini yake.
Ripoti za kutoka England zinafichua vinara hao wa Serie A, Napoli wanamfukuzia kwa karibu supastaa huyo wa Manchester City, aliyenunuliwa kwa pesa nyingi Pauni 100 milioni, ili kwenda kucheza kwenye timu yao kuanzia msimu ujao.
Kocha wa Napoli, Antonio Conte ni shabiki mkubwa wa winga Grealish, ambaye amekuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza huko Man City inayonolewa na Mhispaniola, Pep Guardiola.
Conte anamtaka Grealish kama mchezaji muhimu wa kuingia katika kikosi chake, akiamini atafanya vizuri kama alivyokuwa Aston Villa, licha ya kutokuwa na nyakati nzuri kwa kipindi chake alichokuwa Etihad.
Grealish mwenyewe anatambua kuondoka Etihad kunaweza kumfanya kwenda kuwa na makali ya kutisha kwingine ili kuamsha matumaini ya kuichezea timu yake ya taifa.
Lee Kang-In
ARSENAL imeripotiwa kuwa na mpango wa kuvamia kwenye klabu ya Paris Saint-Germain kwenda kunasa huduma ya kiungo, Lee Kang-In. Kocha Mikel Arteta alianza kumfukuzia staa huyo wa Korea Kusini tangu dirisha la Januari na sasa anataka kumpa kazi bosi mpya wa usajili wa miamba hiyo ya Emirates, Andrea Berta kuhakikisha ananasa huduma ya kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 ili kwenda kuongeza nguvu kwenye kikosi kwa ajili ya kusaka mataji msimu ujao.
Jonathan Tah
NEWCASTLE United imejiingiza kwenye mbio za kuifukuzia huduma ya staa wa Kijerumani, Jonathan Tah dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya. Tah, 29, atapatikana bure mwishoni mwa msimu huu na kuna timu kibao zinahitaji huduma yake. Beki huyo wa kati wa Bayer Leverkusen, Tah amekuwa kwenye rada za klabu nyingine ikiwamo Manchester United, Real Madrid, Barcelona na Bayern Munich. Lakini, Newcastle unamwona kama mbadala wa Marc Guehi wa Crystal Palace.
Moise Kean
MANCHESTER United imeripotiwa kupiga hesabu za kumsajili straika wa Fiorentina, Moise Kean dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi Ulaya. Kean, 25, amekuwa na kiwango bora sana kwenye kikosi cha Viola akirejea makali yake ya zamani ya kufunga mabao baada ya kutikisa nyavu mara 17 na kuasisti tatu katika mechi 30 alizocheza kwenye 30 tangu alipojiunga na timu hiyo dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana.
William Saliba
ARSENAL imeripotiwa kuanzisha mazungumzo na beki wa kati, Wiliam Saliba kumwongeza mkataba mpya ili kuzikata maini klabu zinazomtaka ikiwamo Real Madrid. Arsenal inataka kumzuia Saliba, 24, hata kama anataka kuondoka, asifanye hivyo kwa pesa ndogo kutokana na mkataba wake kufika ukomo 2027. Kwa muda mrefu, Madrid imekuwa ikihusishwa na beki huyo ili kuifanya kuwa na timu ya kibingwa zaidi.
Liam Delap
ARSENAL imeripotiwa kuongeza nguvu zaidi kwenye mchakamchaka wa kuwania saini ya straika wa Ipswich Town, Liam Delap dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Delap amefunga mabao 12 na kuasisti mara mbili kwenye mechi 34 alizochezea Ipswich Ligi Kuu England, ambayo itacheza Championship msimu ujao baada ya kushuka daraja. Kiwango cha fowadi huyo ndicho kitu kinachofanya timu nyingine kuhitaji saini yake.
Alessandro Bastoni
RAIS wa Real Madrid, Florentino Perez ameripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili beki wa kati wa Inter Milan, Alessandro Bastoni dirisha lijalo la uhamisho. Bastoni, 26, amekuwa mchezaji muhimu Inter Milan msimu huu, akicheza mechi 50 za michuano yote, akifunga mara moja na kuasisti tano. Bastoni alicheza kwa kiwango bora wakati Inter ilipoitupa nje Barcelona.
Patrik Schick
CHELSEA, Manchester United na Arsenal zimeingia vitani kufukuzia huduma ya straika wa Bayer Leverkusen, Patrik Schick, 29, dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi. Timu hizo kila moja imeonyesha kuhitaji mshambuliaji wa kati kwenye dirisha lijalo na matokeo yake zimejikuta zikiangukia kwa mchezaji mmoja ambaye amekuwa akifanya vizuri kwenye Bundesliga msimu huu.