Hawa Liverpool kama vipi wapewe tu!

Muktasari:
- Pengo la pointi baina ya Liverpool na timu nyingine kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita limeongezeka baada ya kuichapa 3-1 Southampton, na Arsenal kuangusha pointi kwa kutoka sare ya 1-1 na Manchester United. Liverpool imebakiza mechi tisa na hakuna timu ilishindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuongoza kwa pengo kubwa hivyo la pointi katika hatua kama hii.
LIVERPOOL, ENGLAND: LIVERPOOL imeweka pengo la pointi 15 kileleni kwenye msimamo wa Ligi Kuu England na hilo linafanya kikosi hicho cha Arne Slot kusogelea ubingwa.
Pengo la pointi baina ya Liverpool na timu nyingine kwenye Ligi Kuu England wikiendi iliyopita limeongezeka baada ya kuichapa 3-1 Southampton, na Arsenal kuangusha pointi kwa kutoka sare ya 1-1 na Manchester United. Liverpool imebakiza mechi tisa na hakuna timu ilishindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuongoza kwa pengo kubwa hivyo la pointi katika hatua kama hii.
Ili Arsenal waipiku Liverpool kwenye ubingwa, itahitaji kushinda mechi zote 10 walizobakiza kwenye ligi, huku wakiomba Liverpool ipoteza mechi tano. Na tamu zaidi, Liverpool itakuwa mwenyeji wa Arsenal kwenye mchezo utakaofanyika Mei 10, lakini hadi wakati huo bingwa atakuwa ashapatikana.
Tarehe ya mapema zaidi Liverpool inaweza kuthibitishwa kuwa mabingwa ni Aprili 12 endapo kama itashinda mechi zao mbili zijazo dhidi ya Everton na Fulham huku Arsenal ipoteze kwa Chelsea, Fulham na Everton na kisha iangushe pointi mbele ya Brentford.
Kama Arsenal itapoteza kiporo chake dhidi ya Chelsea, kisha Liverpool ikashinda mechi zake, itabeba taji hilo ikiwa bado na mechi nne wakati itakapokabiliana na Tottenham, Aprili 27. Kama Arsenal itashinda kiporo hicho na kisha ikapata matokeo kama ya Liverpool, basi chama hilo la Slot, linaweza kutangazwa mabingwa wikiendi ya Mei 3/4 itakapocheza na Chelsea.
Tukio jingine ni kwamba Liverpool inaweza kuthibitishwa kuwa mabingwa endapo itashinda dhidi ya Arsenal wakati huo ikiwa mbele kwa pointi saba na mechi zitakuwa bado mbili msimu kumalizika. Hata hivyo, haitakabidhiwa taji lake hadi hapo kwenye mechi yao ya nyumbani dhidi ya Crystal Palace, Mei 25. Hiyo itakuwa mara ya kwanza kwa mashabiki wa Liverpool kushuhudia mubashara timu yao ikikabidhiwa taji tangu mwaka 1990, baada ya lile la 2020 kukabidhiwa bila ya mashabiki kutokana na janga la Uviko -19.
MECHI ZIJAZO
Liverpool: Everton (nyumbani), Fulham (ugenini), West Ham (nyumbani), Leicester City (ugenini), Tottenham (nyumbani), Chelsea (ugenini), Arsenal (nyumbani), Brighton (ugenini), Crystal Palace (nyumbani).
Arsenal: Chelsea (nyumbani), Fulham (nyumbani), Everton (ugenini), Brentford (nyumbani), Ipswich Town (ugenini), Crystal Palace (nyumbani), Bournemouth (nyumbani), Liverpool (ugenini), Newcastle (nyumbani), Southampton (ugenini).