Hawa hapa makipa wanaodaka sana England

LONDON, ENGLAND. KUNA jina moja tu la kipa lililojitokeza kwenye orodha ya mastaa wanaowania tuzo ya Ballon d’Or 2021.

Ni jina la Mtaliano, Gianluigi Donnarumma, anayedakia chama la matajiri wa Ufaransa, Paris Saint-Germain.

Jambo hilo limemshangaza staa wa Liverpool, Sadio Mane aliyehoji kwanini kipa namba moja wa Chelsea, Edouard Mendy hayumo kwenye orodha hiyo licha ya kwamba anadaka sana na msimu uliopita aliwapa The Blues ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mendy anadaiwa kuwa ndiye kipa bora kabisa kwenye Ligi Kuu England kwa sasa na ilishangaza kuona Msenegali huyo hayupo kwenye kinyang’anyiro cha Ballon d’Or.

Wakati Ligi Kuu England ikizidi kunoga, hawa hapa makipa 10 ambao wanatajwa mmojawapo atanyakua tuzo ya ubora kwa msimu huu kutokana na namna walivyoanza kwa kuwakazia washambuliaji wasitikise nyavu zao kirahisi.


10) Illan Meslier - Leeds United

Leeds United ilianza msimu vibaya baada ya kukumbana na vipigo vizito kutoka kwa Manchester United na Liverpool, lakini ushindi wao dhidi ya Watford uliwapa pointi zao tatu za mwanzo. Licha ya kuruhusu wavu wake kuguswa mara 14, ikiwa ni rekodi ya hovyo namba tatu kwenye ligi hiyo msimu huu, yenye wastani wa kuruhusu mabao mawili kwa kila mechi, Illan Meslier ameonekana kubadilika sasa. Staili yake ya udakaji inafananishwa na Thibaut Courtois, akiwa na kimo cha futi 6 na inchi 4, huku akisifiwa kwa uwezo mkubwa wa kuanzisha mashambulizi.


9) Kasper Schmeichel - Leicester City

Kwa miaka mingi, Kasper Schmeichel amekuwa akitambulika kama mtoto wa kipa gwiji, Peter – lakini uwezo wake anapokuwa golini unaeleza bayana kiwango chake kwamba si cha mchezomchezo. Akiwa na umri wa miaka 34, Schmeichel ni mmoja wa makipa mahiri kabisa kwenye Ligi Kuu England, akiwa namba moja Leicester City na makosa yake yamekuwa machache sana. Kiwango cha Schmeichel kimeanza kwa changamoto nyingi katika mechi za karibuni dhidi ya Brighton, Burnley na Crystal Palace – ambapo wapinzani walifunga mabao mawili mawili katika kila mechi.


8) Aaron Ramsdale - Arsenal

Baada ya kushuka daraja akiwa na timu za Bournemouth na Sheffield United, presha ilikuwa kubwa kwelikweli kwa kipa Aaron Ramsdale wakati alipokamilisha uhamisho wake wa Pauni 30 milioni kujiunga na Arsenal kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Akiwa ameruhusu bao moja tu katika mechi zake nne za kwanza kwenye kikosi cha Arsenal, lile moja alilofungwa na Heung-Min Son wa Tottenham, Ramsdale ameonyesha umahiri mkubwa kwenye goli la kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta. Ramsdale alionyesha ubora mkubwa dhidi ya Brighton na kuonyesha kwanini Bernd Leno atakaa benchi.


7) David Raya - Brentford

Brentford imekuwa stori kwenye Ligi Kuu England hadi sasa msimu huu, huku kipa wao David Raya amekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwenye mechi hizo saba zilizochezwa hadi sasa. Uwezo wake wa kupiga pasi ndefu, kutawanya mipira na kuokoa mipira ya hatari kabisa, limewafanya wengi kuitazama Brentford kama timu iliyokuja kivingine kwenye ligi hiyo, huku ikiruhusu mabao sita tu na mechi tatu wakicheza bila ya wavu wao kuguswa. Kwa kiwango cha Raya kinamweka kwenye orodha ya makipa wanaopaswa kudakia timu kubwa zaidi tofauti Brentford.


6) Emiliano Martinez - Aston Villa

Tangu kurejea kwa soka kufuatia janga la virusi vya corona, kumekuwa na mjadala kwamba kipa Emiliano Martinez amekuwa na kiwango bora kabisa golini. Muargentina huyo aliisaidia Arsenal kushinda Kombe la FA kabla ya kwenda kuwa chaguo la kwanza Aston Villa na timu ya taifa ya Argentina. Aliisaidia timu yake ya taifa kushinda Copa America, likiwa ni taji lao la kwanza tangu mwaka 1993 – na amekuwa kwenye kiwango bora kabisa katika kikosi cha Dean Smith. Ubora wake ndani golini, Martinez kwa sasa anahesabika kama mmoja wa makipa mahiri kabisa kwenye Ligi Kuu England.


5) Ederson - Manchester City

Kipa mwingine ambaye utashangaa kwanini hashiki namba moja ni huyu Ederson. Ni mahiri, lakini shida inakuja sehemu moja tu, anachezea Manchester City ambayo imekuwa ikimiliki mpira mara nyingi na Ederson amekuwa hana kazi nzito sana ya kuifanya. Man City imekuwa moja ya timu zenye safu nzuri ya mabeki, ambapo katika mechi saba ilizocheza kwenye ligi hadi sasa imeruhusu mabao matatu tu, hivyo Ederson amekuwa na ulinzi wa kutosha kwa staili ya uchezaji ya kikosi hicho cha Pep Guardiola ya kujilinda kwa kukaa na mpira muda mwingi. Ederson amekuwa hana purukushani nyingi golini Man City.


4) David De Gea - Manchester United

Kuibuka kwa Dean Henderson huko Manchester United na kushuka kiwango kwa David De Gea mwishoni mwa msimu uliopita, kulizua hofu kama Mhispaniola huyo angerudi kuwa namba moja Old Trafford msimu huu. De Gea hakudaka wala kuzuia mkwaju wowote wa penalti kati ya 11 zilizopigwa dhidi yake dhidi ya Villarreal kwenye fainali ya Europa League msimu uliopita. Lakini, msimu huu, Mhispaniola huyo amerudi kwenye ubora wake, akikoa hatari ambazo Man United ingefungwa mabao. Amekuwa moto golini, akidaka pia penalti ya Mark Noble kwenye ligi msimu huu.


3) Robert Sanchez - Brighton

Kipa, Robert Sanchez alicheza mechi yake ya kwanza kwenye ligi hata mwaka mmoja bado haijafika, Novemba 2020 –na sasa amekuwa na uhakika wa kuchaguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Hispania. Timu zake za huko nyuma alicheza kwa mkopo Rochdale na Forest Green Rovers, lakini kwa sasa panga pangua amekuwa namba moja kwenye goli la Brighton akifanya mambo makubwa kwenye mechi za Ligi Kuu England. Tayari Sanchez ana mechi tatu alizocheza bila ya kuruhusu bao msimu huu, huku timu yake ikiruhusu wavu wake kuguswa mara tano tu katika mechi saba. Umri wake ni miaka 23 tu.


2) Alisson Becker - Liverpool

Alisson Becker alishuka kiwango msimu uliopita baada ya kukabiliwa na matatizo binafsi, lakini kwa sasa ameonekana kurudi kwenye ubora wake. Kipa huyo amekuwa na uwezo mkubwa sana wa kusoma mwenendo wa mchezo, huku akiokoa hatari nyingi ambazo timu yake ingefungwa mabao na kupoteza mechi. Alionyesha kiwango bora kabisa kwenye mechi ya sare dhidi ya Manchester City, lakini alitoa mchango mkubwa kwenye mechi za ushindi dhidi ya Norwich, Burnley na Leeds. Ili Liverpool kujihakikishia ubingwa wa ligi, watahitaji huduma ya kipa huyo wa zamani wa AS Roma ikwenye goli lao.


1) Edouard Mendy - Chelsea

Chelsea imekuwa timu yenye ukuta mgumu kwenye Ligi Kuu England na kipa Edouard Mendy amekuwa na mchango mkubwa kwelikweli. Kipa huyo Msenegali, Mendy amekuwa akionyesha ubora wake mkubwa chini ya kocha Thomas Tuchel, ambapo kwa msimu uliopita aliipa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya timu ya Chelsea huku akilinga goli lake kutoguswa. Mendy alikaribia kuacha soka, kabla ya kurudi zake kwenye mchezo na kuwa kipa ambaye mshambuliaji yeyote akifanikiwa kumfunga basi inakuwa furaha kubwa kwake. Kwa msimu huu, Mendy amecheza bila ya kuruhusu wavu wake kuguswa kwenye mechi dhidi ya Aston Villa, Tottenham na Crystal Palace.