Havertz ndiye mwenye shoo yake Arsenal

Muktasari:

  • Arsenal iliichapa The Blues mabao 5-0, shukrani kwa mabao ya Leandro Trossard na ya Ben White na Havertz, ambao kila mmoja alifunga mara mbili katika mchezo huo.

LONDON, ENGLANG: Kai Havertz, ndiye steringi wa mchezo kwa sasa akisimamia shoo za Arsenal, ikipambana jino kwa jino kwenye kufukuzia ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu na kushusha kipigo kizito kwa Chelsea.


Arsenal iliichapa The Blues mabao 5-0, shukrani kwa mabao ya Leandro Trossard na ya Ben White na Havertz, ambao kila mmoja alifunga mara mbili katika mchezo huo.


Havertz alikuwa na wakati mgumu mwanzoni mwa maisha yake huko Emirates baada ya kunaswa kwa pesa nyingi kutoka Chelsea, lakini kwa sasa amejipata na kila kitu kinakwenda vizuri kisawasawa.


Bao lake la pili alilofunga dhidi ya Chelsea lilikuwa la 12 msimu huu baada ya mechi 47 huku akifanya mipango mingi ya Arsenal ndani ya uwanja kwenda sawa kuliko ilivyotarajiwa miezi michache iliyopita. Havertz, 24, amehusika kwenye mabao mengi sana ya Arsenal kwa miezi ya hivi karibuni.


-Mavitu yake pale mbele; Kocha Mikel Arteta awali alikuwa akimpanga Havertz upande wa kushoto kwenye safu ya viungo watatu, alishindwa kuonyesha cheche. Lakini, kwa sasa ameamua kumtumia mbele kabisa kwenye safu ya ushambuliaji, eneo ambalo Mjerumani huyo amelitendea haki. Arsenal imefunga mabao 26 tangu Havertz alipoanza kutumika kwenye safu ya ushambuliaji.


-Kiunganishi uwanjani; Havertz hafanyi vizuri tu kwenye mabao, bali amekuwa kiunganishi kizuri kwa wachezaji wenzake kuwasaidia kufunga mabao. Amekuwa akituliza kasi ya mchezo na wakati mwingi-ne anashuka chini hadi kwenye eneo la viungo kwenda kutengeneza munganiko mzuri na viungo Martin Odegaard na Declan Rice.


-Mwamba wa kukaba; Arsenal imekuwa mafundi wa kunasa mipira na kuifanya kuwa na faida kwa maana ya kuigeuza kuwa mabao kwenye msimu huu. Na jambo hilo limedaiwa kufanywa vizuri na Havertz, ambaye amekuwa hodari kwenye kukaba na kunyang’anya mipira ambayo imekuwa na faida kubwa kwa timu yake.


-Mikimbio ya kiufundi; Havertz amekuwa akiwavuruga mabeki wa timu pinzani kutokana na mikimbio yake ya kiufundi wakati anapopiga pasi kwa wachezaji wa pembeni Bukayo Saka na Gabriel Martinelli. Havertz anapoona mipira ipo kwa wachezaji hao wa pembeni, amekuwa na mikimbio ya kupita nyuma ya mabeki wa timu pinzani na kuwavuruga kabisa kunakoruhusu wachezaji wenzake wa Arsenal kufunga..