Hamilton alia na afya yake ya akili
Muktasari:
- Bingwa huyo wa dunia mara saba amekuwa na matatizo ya afya ya akili tangu alipokuwa na umri wa miaka 13.
DEREVA wa Formular 01, Lewis Hamilton amefichua kuwa amekuwa na msongo wa mawazo kutokana presha anapokuwa anashindana kwenye mashindano mbalimbali ya magari.
Bingwa huyo wa dunia mara saba amekuwa na matatizo ya afya ya akili tangu alipokuwa na umri wa miaka 13.
“Nadhani ilikuwa msongo wa mawazo uliosababishwa na mbio za magari, lakini pia uonevu ambao nilikutana nao nikiwa shule,” alisema dereva huyo.
Lewis mwenye umri wa miaka 39 alisema kuna kipindi alikuwa akiamka saa 11:00 alfajiri akiwa na msongo wa mawazo na alijilazimisha kukimbia kilomita 10 kila asubuhi ili kujaribu kuweka akili y sawa.
Dereva huyo pia alifunguka kwamba kuna muda alilazimika kuchukua mapumziko na kujitenga sehemu ambayo hakuna mzunguko wa watu ili atulize akili.
“Niliwahi kuzungumza na mwanamke mmoja miaka iliyopita juu ya hali hii, lakini hiyo haikusaidia bado,” alisema mkali huyo.