Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gyokeres anapoingizwa kwenye umafia wa soka la Ulaya

MAFIA Pict

Muktasari:

  • Wiki hii imesambaa sana stori ya straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres akidaiwa amekasirishwa na viongozi wa timu hiyo ambao wamegoma kuendana na makubaliano waliyowahi kuweka Januari mwaka huu.

RAFIKI yangu mmoja, wakala wa wachezaji wa mpira wa miguu, aliwahi kuniambia, ‘Football is a mafia game’, niliposhtuka alinifafanulia haikuwa na maana ni umafia wa watu kuwindana na kupotezeana maisha, bali mambo tu yasiyoumiza yanayofanyika humo ndiyo umafia wenyewe.

Wiki hii imesambaa sana stori ya straika wa Sporting Lisbon, Viktor Gyokeres akidaiwa amekasirishwa na viongozi wa timu hiyo ambao wamegoma kuendana na makubaliano waliyowahi kuweka Januari mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti, wakala na Gyokeres walikubaliana na Sporting mchezaji huyo angeondoka kwa ada ya Euro 80 milioni tofauti na ile ya Euro 100 milioni ambayo ipo katika mkataba wake, sasa mambo yamebadilika na Sporting inataka yote.

Rais wa timu hiyo, Frederico Varandas amejitokeza hadharani akisema hakuwahi kufanya makubaliano na upande wa mchezaji Gyokeres ataondoka kwa Euro 80 milioni, bali alikubaliana nao kiasi kilichopo katika mkataba sio lazima kifikiwe, hivyo anaweza kuondoka kwa ada ya chini ya Euro 100 milioni na akasisitiza msimamo wake ndiyo huo na hautobadilika.

Rudi nyuma, makubaliano haya wakati yanawekwa Januari mwaka huu ilikuwa ni sehemu ya ahadi baada ya mchezaji kukubali kuendelea kuichezea timu hiyo licha ya kuwepo kwa ofa kutoka kwa timu iliyokuwa tayari kuvunja mkataba wake.

Hivyo, hiki kinachoendelea kwa Gyokeres unaweza kuona kama ni usaliti licha ya yeye kuonyesha uungwana wakati ule, hapana.

Mara nyingi hivi ndivyo mpira unavyokuwa, ni mchezo wa ukatili sana, siyo tu ndani ya uwanja hata nje ya uwanja.

Kule Amerika ya Kusini au Kaskazini, matukio ya wachezaji kupigwa risasi baada ya kuchomesha timu au kucheza vibaya ni mengi sana, lakini Ulaya, umafia wa mpira upo kwenye shughuli kama hizi za usajili.

Mwaka jana, Leny Yoro na wakala wake walikuwa katika mazungumzo na Real Madrid, wakafanya hadi makubaliano binafsi, ada ya uhamisho ya mchezaji kwa mujibu wa mkataba wake haikuwa inazidi Euro 50 milioni.

Madrid walikuwa tayari kuilipa lakini ghafla wakati mambo yanaenda vizuri, Manchester United ikakaa mezani, ikaweka ada ya uhamisho ambayo ilikuwa inavuka kile kipengele cha mkataba wa mchezaji huyu. Nice ikachanganyikiwa, Leny akashikilia msimamo wake anataka kwenda Madrid, ilikuwa ndiyo ndoto yake.

Mabosi wa Nice wakakaa kikao, wakajadili wakapata jibu. Wao walikubali ofa ya Man United na licha ya mchezaji kugoma wakamwambia akiendelea kushikilia msimamo wa kucheza Madrid, wao hawatomuuza huko na katika mwaka wake mmoja uliosalia katika mkataba wake hawatomchezesha hata mechi moja msimu mzima.

Leny akaomba yaishe akakubali kuchutama akaenda zake Man United.

Matukio ni mengi, ya kufurahisha na kuhuzunisha. Hivyo ndivyo ilivyo dunia ya mpira pale Ulaya.

Wakati Waarabu wa PSG wanatoa pesa ya kumnunua Neymar kwa Euro 222 milioni, walifahamu sheria za masuala ya kifedha zisingeweza  kuwaruhusu kutoa kiasi hicho na kufanya usajili wake ambao hadi leo umeendelea kuwa ghali zaidi duniani, walichokifanya ni kumwingizia pesa zote Neymar katika akaunti yake, kisha yeye ndio akaenda kuununua mkataba wake na kuuvunja, akawa huru wakamsajili.

Muda mwingine inapendeza sana ukiwa unaziangalia hizi drama. Ukiwa umezubaa kidogo tu, unajikuta umenyakuliwa na hujui umenyakuliwaje.

Siku moja wakati Chelsea inamsajili William kutoka Urusi ni Tottenham ndio iliyolipa hadi nauli yake ya ndege kwenda London, alipofika uwanja wa ndege, Chelsea wakamfungulia Range wakamwambia panda hii tukupeleke katika ofisi za timu(Spurs), ukasaini, bahati mbaya au nzuri gari ikaenda Stamford Bridge, Spurs hawasahau hata kidogo tukio lile.

Lakini ndivyo ilivyo, mpira wa miguu wa Ulaya una umafia wake ndo kama huu.

Wakati fulani,Sir Alex Ferguson alikaribia kumwaga machozi baada ya John Obi Mikel kumtoroka katika mazingira ya kutatanisha na kwenda kusaini Chelsea, lakini yeye pia aliwahi kumpora Cristiano Ronaldo katika mdogo wa Arsene Wenger.

Ndivyo ulivyo, ndo utamua wa mpira wa miguu, usipokufurahisha kiwanjani subiria kipindi kama hiki, mambo huwa ni mengi sana.