Gwiji wa Southampton anusurika kifo Uholanzi
Muktasari:
- Winga huyo wa zamani wa Southampton, ambaye aliwahi kununua gari la kifahari aina ya Lamborghini Urus lenye thamani ya Sh864 milioni, alihusika katika ajali ya kutisha ya magari matatu kwenye barabara kuu ya A4 karibu na jiji la Leiden, Uholanzi.
Mchezaji wa zamani wa Ligi ya EPL, Eljero Elia, amenusurika kifo baada ya ajali mbaya iliyohusisha magari matatu nchini Uholanzi.
Winga huyo wa zamani wa Southampton, ambaye aliwahi kununua gari la kifahari aina ya Lamborghini Urus lenye thamani ya Sh864 milioni, alihusika katika ajali ya kutisha ya magari matatu kwenye barabara kuu ya A4 karibu na jiji la Leiden, Uholanzi.
Kwa mujibu wa taarifa za polisi, hakuna aliyejeruhiwa vibaya katika ajali hiyo, lakini madereva wawili walichukuliwa na kupelekwa kituoni. Elia, mwenye umri wa miaka 38, pia alichukuliwa na gari la polisi akiwa na mwanaume mwingine kwa ajili ya kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia jana Jumamosi Oktoba 4, 2025 saa 9:45 usiku kwa saa za Uholanzi.
Elia amehojiwa na kituo cha habari cha Omroep West na kueleza kuwa gari lake liliteleza baada ya kujaribu kusimama ghafla.
Amesema: "Nilikuwa naendesha katika eneo ambalo kwa kawaida huwa tulivu kwa wakati huo. Ghafla nikaona magari mbele yangu yakisimama. Nilijaribu kusimama, lakini gari langu likateleza."
Elia pia amefichua alichowaambia polisi alipokuwa akihojiwa: "Niliwaeleza polisi kilichotokea, kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani."
Vyombo vya habari vya eneo hilo vimeripoti kuwa madereva wa magari mengine mawili waliokumbwa na ajali hiyo walikamatwa na kupelekwa kufanyiwa vipimo, huku polisi wakitaka kubaini kama walikuwa wamekunywa pombe.
Elia alijiunga na Southampton kwa mkopo Januari 2015 na kucheza mechi 17, akifunga mabao mawili. Hata hivyo, klabu hiyo haikumchukua kwa mkataba wa kudumu na alirudi Werder Bremen ya Ujerumani.
Mholanzi huyo pia amewahi kuchezea klabu za Juventus, Feyenoord, FC Twente na ADO Den Haag. Aliichezea timu ya taifa ya Uholanzi mara 30 na kufunga mabao dhidi ya Scotland na Hungary.
Elia alitangaza kustaafu soka mwaka 2022 baada ya kuumia kifundo cha mguu.