Gwiji wa Argentina akibashiria neema kikosi cha Lionel Scaloni
Muktasari:
- Argentina inakwenda kwenye fainali hizo zitakazounguruma nchini Mexico, Marekani na Canada, ikiwa kama bingwa mtetezi wa michuano hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.
Mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Argentina, Gabriel Batistuta, amebashiri kuwa ‘Albiceleste’ itacheza mechi ya fainali katika michuano ya Kombe la Dunia 2026.
Argentina inakwenda kwenye fainali hizo zitakazounguruma nchini Mexico, Marekani na Canada, ikiwa kama bingwa mtetezi wa michuano hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.
Batistuta anaamini kwamba, wachezaji wa kocha Lionel Scaloni wako katika hali ya utulivu, na kikosi hicho ni bora zaidi kuliko kilivyokuwa wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.
Gwiji huyo ambaye aliitumikia Argentina katika mechi 78 na kufunga mabao 54, ametoa ubashiri huo kabla ya droo ya Kombe la Dunia 2026 itakayo fanyika leo Ijumaa, Desemba 5, 2025 nchini Marekani.
“Sasa hivi, kikosi cha Argentina kipo kwenye hali ya ubora. Wachezaji wetu wanajua namna wanavyotaka kucheza, na wako kwenye tulivu kwa sababu wanajua ni jinsi gani ya kushinda kila mechi. Nina uhakika watafika fainali tena,” amesema Batistuta katika mahojiano na TyC Sports.
Timu ya taifa ya Argentina imepangwa katika Pot 1 kwenye upangaji wa makundi ya Kombe la Dunia 2026. Hii inatokana na rekodi na nafasi ya juu katika viwango vya ubora vya FIFA.
Kwa nafasi hiyo, Argentina itakuwa miongoni mwa timu zinazochukuliwa kuwa na nguvu na kushirikishwa katika makundi yenye ushindani, huku ikitarajiwa kuepuka kukutana na timu zingine zilizoko Pot 1 katika hatua ya makundi.
Kuanzia hapa, Argentina itakuwa na nafasi nzuri ya kupanga mipango yao ya mashindano na kuanza kampeni ya kutetea taji la Kombe la Dunia, likiwa ni baada ya ushindi wao wa Kombe la Dunia 2022, hii inawapa wachezaji wa Lionel Scaloni hamasa na uhakika wa kuendelea kushindana kwa kiwango cha juu msimu ujao.