Greenwood kurudi? Bado sana unaambiwa

MANCHESTER, ENGLAND.LICHA ya kesi ya Mason Greenwood kufutwa na mahakama ya Greater Manchester, klabu ya Manchester United imesisitiza kinda huyo hatarudi mpaka uongozi utakapojidili suala lake kabla maamuzi kutolewa.

Greenwood alikuwa akituhumiwa na mashtaka ya kutishia kuua na ubakaji dhidi ya mpenzi wake Harriet Robson hata hivyo ameachiwa huru baada ya kesi kufutwa. Winga huyo alikamatwa na polisi akiwa nyumbani kwao tangu Januari mwaka jana kwaajili ya uchunguzi wa tuhuma hizo zilizokuwa zikimkabili.

Ikumbukwe Greenwood alitinga mahakamani kwa mara ya kwanza Novemba mwaka jana lakini kesi hiyo ikahairishwa na ingesikilizwa tena Novemba 23 mwaka huu. Aidha uongozi wa Man United umethibitisha kwasasa hatazungumza chochote kuhusu mustakabali wa Greenwood hadi uchunguzi wao utakapomilika kuhusiana na sakata zima.

"Tunaelewa kesi iliyokuwa ikimhusu Mason Greenwood imefutwa, sasa klabu itakaa na kuchanganua suala hili kabla ya hatua nyingine inayofuata," ilibainisha taarifa ya klabu ya Man United.

Baada ya kesi hiyo kufutwa Greenwood alizungumza kwa mara ya kwanza akidai anashukuru ishu yake imemalizika salama. Akisema: "Nimefurahi kila kitu kimemalizika, nawashukuru familia yangu na marafiki zangu kwa ushirikiano wao walionipa, sitazungumza kingine zaidi kwasasa."

Jina la Greenwood bado lipo kwenye orodha ya wachezaji wa kikosi cha kwanza kupitia tovuti yao maalumu hata hivyo hataruhusiwa kurudi kikosini mpaka uongozi utakapotoa maamuzi. Greenwood mwenye umri wa miaka 21 alikuwa tegemeo katika kikosi cha Man United kutokana uwezo wake wa kupachika mabao, kinda huyo alifananishwa na Robin van Persie aina ya uchezaji wake kwasababu anatumia miguu yote miwili kama ilivokuwa Mdachi huyo.

Mara ya mwisho Greenwood kuonekana uwanjani ilikuwa katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya West Ham United, ambapo Man United iliibuka na ushindi wa bao 1-0, Januari 22 mwaka jana.