Grealish ampeleka Bellingham Etihad

MANCHESTER, ENGLAND. KIUNGO wa Manchester City, Jack Grealish amewapagawisha mashabiki kutokana na komenti yake inayomshinikiza Jude Bellingham ajiunge na timu hiyo.

Wawili hao wanafahamiana kwa muda mrefu kwasababu wanacheza pamoja timu ya taifa ya England, huku Grealish akitumia mwanya huo kumshawishi Bellingahm ambaye anakipiga Borussia Dortmund.

Vile vile Bellingham na Grealish wana ukaribu na beki wa Man City, Manuel Akanji ambaye ametokea Borrusia Dortmund msimu uliopita sasa anataka kinda huyo ahamie Etihad.
Sasa Grealish alivamia mazungumzo ya Bellingham na mchezaji mwenzake wa Borrusia Dortmund, Gio Reyna kupitia akaunti yake ya Instagram akidai "Njoo Man City" na kupagawisha mashabiki waliokuwa wakifatilia chati zao.

Grealish ni shabiki mkubwa wa Bellingham na alianza kumkubali tangu alipoibuka kuwa kinara wa mchezo, England ilipocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Ivory Coast mwaka jana.
Winga huyo alimsifia Bellingam mwenye umri wa miaka 19 akidai kinda huyo ana kipaji kikubwa cha kucheza soka.

Hata hivyo Man City itapata wakati mgumu kunasa saini yake kwasababu Manchester United inamfukuzia kiungo huyo. Kwa mujibu wa ripoti Erik ten Hag anamkubali na atapambana kuhakikisha Bellingham anatua Old Trafford msimu ujao.
Vile vile ripoti zimeripoti Liverpool imeingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania saini ya Bellingham  baada ya Jurgen Klopp kupeleka mapendekezo kwa mabosi.