Singida Black Stars yaanza kuzidai pesa za Gomez

Muktasari:
- Inadaiwa kuwa, tayari Singida BS imetoa siku 14 kwa Wydad kutekeleza makubaliano yao ya kuuziana mchezaji huyo kabla haijakimbilia Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutokana na ukiukaji wa malipo.
MABOSI wa Singida Black Stars wameiandikia barua Wydad Casablanca ya Morocco kudai malipo ya mauzo ya mshambuliaji, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ waliyemuuza kupitia dirisha dogo la usajili akitokea Fountain Gate aliyokuwa akiitumikia kwa mkopo.
Inadaiwa kuwa, tayari Singida BS imetoa siku 14 kwa Wydad kutekeleza makubaliano yao ya kuuziana mchezaji huyo kabla haijakimbilia Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kutokana na ukiukaji wa malipo.
Gomez aliyesaini mkataba wa miaka minne na nusu kuitumikia Wydad inayoshiriki Ligi Kuu ya Morocco alisajiliwa kwa ada ya uhamisho ya Sh 891 milioni na mshahara kwa mwezi unaotajwa kufikia Sh6 milioni, huku kukiwa na bonasi kila akifunga bao.
Chanzo cha kuaminika kutoka Singida BS kimeliambia Mwanaspoti, Wydad imeshindwa kutimiza kile ilichoahidi juu ya malipo ya kiasi cha fedha walichokubaliana kwenye biashara ya kumpata mchezaji huyo.
“Taarifa hizo ni za kweli lakini ni siri baina ya klabu yetu na timu tuliyofanya nayo biashara hatukutarajia haya yatatoka nje kwani mipango ni kumalizana sisi wenyewe kama biashara ilivyofanyika lakini ni ukweli uliousikia,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini;
“Sisi ni klabu, bado tutakuwa na biashara nyingine nyingi sio vyema jambo hili la makubaliano baina yetu kuvuja, ila tukishindwana ndio tutaweka kila kitu wazi kuomba msaada wa kutoa taarifa kwa sasa ni mazungumzo ya ndani yanafanyika juu ya barua ni kweli imetumwa.”
Nyota huyo amecheza Ligi Kuu Bara nusu msimu baada ya kufanya vizuri katika kikosi cha KVZ ya Zanzibar na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Zanzibar msimu wa 2023/2024 akifunga mabao 20 na kutoa pasi za mabao saba (asisti) katika michezo 27 aliyocheza kati ya 30.