Gordon aziingiza vitani Arsenal, Liverpool
Muktasari:
- Gordon ameonyesha kiwango bora msimu huu, hali iliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia zaidi sokoni na Arsenal pamoja na Liverpool kwa sasa zinapambana sana kusuka safu zao za ushambuliaji.
ARSENAL ipo tayari kuingia vitani na Liverpool ili kumsajili mshambuliaji wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Anthony Gordon, 25, dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Gordon ameonyesha kiwango bora msimu huu, hali iliyomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia zaidi sokoni na Arsenal pamoja na Liverpool kwa sasa zinapambana sana kusuka safu zao za ushambuliaji.
Mara kadhaa Newcastle imeripotiwa kuwa haipo tayari kumuuza Gordon kwa bei rahisi ikitajwa wanahitaji walau Pauni 100 milioni ili kufanya hivyo.
Uwepo wa timu hizo mbili unaonekana huenda ukasababisha Gordon auzwe kwa zaidi ya Pauni 100 milioni ambayo Newcastle inaihitaji.
Mkataba wa fundi huyu unatarajiwa kumalizika mwaka 2030 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 45 za michuano yote, amefunga mabao 17 na kutoa asisti tano.
Mbali ya ada ya uhamisho, Gordon pia anahitaji mshahara unaokaribia Pauni 300,000 kwa wiki ambao ni mara mbili ya mshahara wake wa sasa wa Pauni 150,000.
Valentin Barco
CHELSEA imeonyesha nia ya kumsajili beki wa kimataifa wa Argentina, Valentin Barco, 21, kutoka RC Strasbourg Alsace ambayo pia inamilikiwa na wamiliki wao.
Kwa asilimia kubwa Barco anaonekana kuwa karibu kutua Chelsea kwani mabosi wa Chelsea ndio wenye maamuzi ya wapi staa huyo aende kwa kuwa wana hisa pia Strasbourg.
Dili hilo ni sehemu ya mkakati wa Chelsea kuendelea kusuja kikosi chao kupitia wachezaji vijana. Mkataba wake unamalizika mwaka 2029.
Guglielmo Vicario
INTER Milan inamnyatia kipa wa Tottenham Hotspur na timu ya taifa ya Italia, Guglielmo Vicario na inamhitaji akawe kipa wao namba moja.
Vicario ameonyesha kiwango kizuri Ligi Kuu England lakini dili la Inter linaonekana kumvutia sana na anataka kujiunga nao.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2028 na msimu huu amecheza mechi 43 za michuano yote na kumaliza 13 bila ya kuruhusu bao.
Marco Palestra
LIVERPOOL inaripotiwa kuwa na mpango wa kumsajili beki wa kulia wa kimataifa wa Italia, 21, Marco Palestra, kutoka Atalanta dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi.
Kwa sasa mazungumzo tayari yameshaanza na kuna uwezekano mkubwa dili hilo likakamilika kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu.
Mkataba wa sasa wa Palestra unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 30 za michuano yote.
Tom Atcheson
MANCHESTER United ni miongoni mwa klabu kadhaa za Ligi Kuu England zinazomfuatilia beki wa Blackburn Rovers na timu ya taifa ya Northern Ireland, Tom Atcheson, 19. Atcheson amekuwa katika rada za timu nyingi za EPL tangu mwaka jana kutokana na kiwango bora alichoonyesha ligi daraja la kwanza licha ya umri wake mdogo.
Hata hivyo, Man United inaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kumpata fundi huyo kwani amewaambia wawakilishi wake kwamba timu pekee anayohitaji kucheza msimu ujao ni Man United na ikishidikana ndio ataenda sehemu nyingine.
Sergio Arribas
SUNDERLAND inaweza kuingia kwenye harakati za kumsajili kiungo mshambuliaji wa UD Almería, Sergio Arribas, 24, dirisha lijalo la majira ya kiangazi baada ya ripoti kudai mkurugenzi wao wa michezo, Florent Ghisolfi, ameshaanza mazungumzo.
Arribas anasifika kwa ubunifu wake jambo linalomfanya kuwa mchezaji anayewindwa sana Ulaya. Iwapo dili hilo litafanyika, Sunderland huenda ikatoa hadi Pauni 30 milioni kama ada yake ya usajili.
Santiago Castro
WEST Ham United na Nottingham Forest zinakutana na ushindani mkali kutoka AC Milan katika harakati zao za kumsajili mshambuliaji wa Bologna na Argentina, Santiago Castro, 21.
Castro ambaye ameendelea kuonyesha makali yake katika Serie A, amekuwa akitazamwa na maskauti wa klabu hizo tajwa tangu mwanzo wa msimu huu.
Inaelezwa West Ham na Forest zinataka kumsajili ili kuimarisha safu zao za ushambuliaji, lakini Milan inaonekana kuwa na nafasi kubwa kwa sasa.
Wesley Franca
ARSENAL bado inafanya mazungumzo mazungumzo na wawakilishi wa staa wa AS Roma na timu ya taifa ya Brazil, Wesley Franca, 22, inayehitaji kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Fofana ambaye kwa sasa ni mmoja kati ya mastaa tegemeo wa kikosi cha kwanza cha Roma, mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2030. Tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 25 za michuano yote na kufunga mabao manne.