Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gibbs-White aonyesha jeraha lake akimtaja mwenzake

GIBBS Pict

Muktasari:

  • Kiungo huyo wa Nottingham Forest alichapisha picha akiwa na nyuzi alizoshonwa kwenye paji la uso wake, zikionyesha ukubwa wa jeraha hilo linalomuweka shakani kucheza katika nusu fainali ya pili ya Europa League dhidi ya Aston Villa, kesho Alhamisi.

LONDON, ENGLAND: KIUNGO wa Nottingham Forest, Morgan Gibbs-White, amewashtua mashabiki baada ya kuonyesha picha ya jeraha lake la kichwa lililojaa mishono kufuatia mgongano mkali na kipa wa Chelsea, Robert Sanchez.

Tukio hilo lilitokea wakati wa ushindi wa kihistoria wa Forest wa mabao 3-1 dhidi ya Chelsea kwenye Uwanja wa Stamford Bridge. Huo ulikuwa mgongano wa pili wa kutisha katika mechi hiyo, baada ya kinda wa Chelsea, Jesse Derry, kutolewa nje kwa machela mapema kipindi cha kwanza.

Gibbs-White, ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba kipindi cha pili, alilazimika kutolewa nje dakika ya 66 baada ya paji lake la uso kupasuka vibaya.

Katika picha aliyoweka kwenye mtandao wa Instagram, nyota huyo ameonekana akiwa na mishono inayotoka kwenye paji la uso hadi juu ya pua, lakini amewatoa hofu mashabiki kwa kuonyesha ishara ya kidole gumba.

GIB 02

"Asanteni kwa ujumbe wenu, ushindi mkubwa! Hongera Taiwo Awoniyi," ameandika Gibbs-White.

Kwa upande mwingine, Robert Sanchez naye alishindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Filip Jorgensen. Sanchez alionyesha uungwana kwa kumtumia ujumbe Gibbs-White akisema: "Nimeona jeraha lako ni baya zaidi kuliko langu, natumai uko sawa mkuu."

Licha ya ukubwa wa jeraha hilo, kocha wa Nottingham Forest, Vitor Pereira, ana matumaini kuwa, kiungo huyo atakuwepo kwenye mchezo muhimu wa nusu fainali ya Europa League dhidi ya Aston Villa keshokutwa Alhamisi.

Pereira amesema: "Nilizungumza naye, anaongea kawaida na anakumbuka kila kitu. Tatizo ni maumivu na jeraha usoni, lakini ni mpiganaji. Nina matumaini idara yetu ya tiba itafanya 'muujiza' ili kumrejesha uwanjani kwa sababu ni mchezaji muhimu sana kwetu."

GIB 01

Forest, ambayo ilifanya mabadiliko ya wachezaji wanane ili kupumzisha baadhi ya wachezaji kwa ajili ya Europa League, ilipata ushindi huo kupitia mabao mawili ya Taiwo Awoniyi na penalti ya Igor Jesus, huku Cole Palmer akikosa penalti upande wa Chelsea. Bao la kufutia machozi la wenyeji likafungwa na Joao Pedro kwa staili ya sarakasi.

Sheria za UEFA zinataka mchezaji aliyepata mshtuko wa ubongo kukaa nje kwa siku sita, lakini Pereira anaamini Gibbs-White hakupata mshtuko huo, bali ni jeraha la nje pekee.