Ghana yaaga Kombe la Dunia, Colombia kuvaana na Uswisi 16 bora
Muktasari:
- Bao pekee la mchezo lilifungwa mapema dakika ya 14 na nyota wa Colombia, Jhon Arias, aliyemalizia vizuri pasi ya Luis Suárez, aliyeingia uwanjani dakika ya nane kuchukua nafasi ya Jhon Córdoba.
KANSAS CITY, MAREKANI: Timu ya Taifa ya Ghana, Black Stars, imeaga Kombe la Dunia 2026 baada ya kuchapwa bao 1-0 na Colombia katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Kansas City, Missouri, Marekani.
Bao pekee la mchezo lilifungwa mapema dakika ya 14 na nyota wa Colombia, Jhon Arias, aliyemalizia vizuri pasi ya Luis Suárez, aliyeingia uwanjani dakika ya nane kuchukua nafasi ya Jhon Córdoba.
Colombia ilitawala mchezo kwa kiasi kikubwa kipindi cha kwanza, ikimiliki mpira kwa asilimia 67 dhidi ya asilimia 33 za Ghana. Mbali na umiliki huo, Colombia ilipiga mashuti matatu yaliyolenga lango, huku moja likizaa bao. Ghana, kwa upande wake, ilishindwa kabisa kupiga shuti lililolenga lango.
Ghana ilinusurika kuruhusu bao la pili dakika ya 56 baada ya Luis Díaz kuifungia Colombia, lakini bao hilo lilibatilishwa na Mfumo wa Msaidizi wa Video wa Waamuzi (VAR) baada ya kubainika kuwa alikuwa ameotea.
Licha ya kuingia kipindi cha pili ikihitaji kusawazisha, Ghana haikuonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji na ilishindwa kutengeneza nafasi za kutosha za kusawazisha. Mpaka mwamuzi alipopuliza filimbi ya mwisho, Colombia ilikuwa imejihakikishia ushindi na tiketi ya kutinga hatua ya 16 Bora, huku Ghana ikiaga rasmi mashindano hayo.
Colombia sasa itakutana na Uswisi katika hatua ya 16 Bora baada ya Uswisi kuifunga Algeria mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Julai 3, 2026. Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Julai 7, 2026 kwenye Uwanja wa BC Place, jijini Vancouver, Canada.
Chini ya Kocha Mkuu Néstor Lorenzo, Colombia imerejea kwenye Kombe la Dunia baada ya kukosa fainali za Qatar 2022. Timu hiyo ilifuzu kwa kumaliza nafasi ya tatu katika michuano ya kufuzu ya Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (CONMEBOL), nyuma ya Argentina na Ecuador.
Maarufu kama Los Cafeteros, Colombia inashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya saba tangu ilipoanza kushiriki mwaka 1962. Lorenzo pia anakumbukwa kwa kuwa sehemu ya kikosi cha Argentina kilichocheza fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1990.
Mafanikio makubwa ya Colombia katika historia ya Kombe la Dunia ni kufika robo fainali mwaka 2014 nchini Brazil, ambako iliondolewa na wenyeji kwa mabao 2-1. Hata hivyo, mashindano hayo yalibaki ya kihistoria kwa Colombia baada ya James Rodríguez kutwaa tuzo ya mfungaji bora kwa mabao sita.
Kwa upande wa Ghana, historia yake bora zaidi katika Kombe la Dunia ilikuja mwaka 2010 nchini Afrika Kusini ilipofika robo fainali kabla ya kutolewa na Uruguay kwa mikwaju ya penalti 4-2, kufuatia sare ya bao 1-1.
Mchezo huo wa Julai 2, 2010, bado unakumbukwa na wengi kutokana na Luis Suárez kuokoa mpira kwa mkono akiwa kwenye mstari wa goli katika dakika ya 120 na kupewa kadi nyekundu.
Hata hivyo, Asamoah Gyan alikosa penalti iliyofuata baada ya mpira kugonga mwamba, na Ghana ikapoteza nafasi ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia.
Ghana ilicheza Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza mwaka 2006 nchini Ujerumani, ilipofuzu hatua ya 16 Bora kabla ya kutolewa na Brazil kwa mabao 3-0.
Tangu mafanikio yake ya mwaka 2010, imekuwa ikikumbana na wakati mgumu, ikitolewa hatua ya makundi katika fainali za 2014 na 2022, kabla ya safari yake ya Kombe la Dunia 2026 kumalizikia hatua ya 32 Bora.