Gazza asimulia alivyorudi duniani kutoka kuzimu
Muktasari:
- Shujaa huyo wa zamani wa England, mwenye umri wa miaka 58, amefunguka kuhusu tukio hilo ambapo moyo wake ulisimama wakati alipokuwa akipambana na uraibu wa pombe katika kliniki moja huko Arizona miaka 12 iliyopita.
GWIJI wa soka nchini England, Paul John Gascoigne maarufu Gazza, amefichua alivyorudi duniani kutoka kuzimu baada ya kufa akiwa kwenye kitanda cha upasuaji alipokuwa katika koma ya muda ya siku 18.
Shujaa huyo wa zamani wa England, mwenye umri wa miaka 58, amefunguka kuhusu tukio hilo ambapo moyo wake ulisimama wakati alipokuwa akipambana na uraibu wa pombe katika kliniki moja huko Arizona miaka 12 iliyopita.
Madaktari walilazimika kumchoma sindano moja kwa moja kwenye moyo ili kuokoa maisha yake.
Nyota huyo alikuwa ameacha pombe ghafla kwa jaribio la kuacha kabisa ulevi. Lakini hali hiyo ilimfanya aingizwe kwenye koma ya matibabu kwa siku 18 kabla ya madaktari kumrudisha kwenye hali yake ya kawaida.
Tukio hilo liliibua uvumi wa uongo kwamba Gascoigne alikuwa amefariki kweli. Na alipopona na kurudi Uingereza, gwiji huyo alimshangaza mwanamke mmoja mtaani ambaye alikuwa ameamini uvumi huo wa kusikitisha.
Akizungumza na The Mirror wakati akitangaza wasifu wake mpya ‘Eight’, nyota huyo wa zamani wa Newcastle, Tottenham na Everton, amesema: “Nikikumbuka kilichotokea Arizona, wakati nikiwa kwenye matibabu, lilikuwa suala la kutisha sana.
“Madaktari walisema waliweza kunirudisha. Nilipozinduka nilikuwa nimejaa dawa kali. Hatimaye nilipiga simu kwenye familia yangu nikawaambia, ‘nimeshinda, nimepona.’
“Lakini ninakumbuka niliporudi Newcastle na kukutana na mwanamke mmoja barabarani, alisimama na kunitazama, karibu azimie.
“Aliniambia, ‘Nilidhani ulikuwa umekufa’. Nikamwambia, ‘Bila shaka sijafa’. Baadaye niligundua watu walikuwa wamepokea ujumbe tofauti kwenye viwanja vya michezo. Walisema nimekufa. Kwa hiyo yule mwanamke alihisi kama ameona mzimu wangu.”
Akikumbuka maisha yake kwenye kliniki ya Arizona, Gazza ameongeza: “Ninaamini kama ningekwenda kwenye kituo kingine chochote, nafikiri ningekufa.
“Sikumbuki mengi yaliyotokea baadaye. Nikirejea kwenye ulevi, huwa naacha ghafla kwa sababu nataka kuhisi maumivu.
“Kule Arizona, ilikuwa ni ya kutisha, lakini sikuhisi madhara kwa sababu nilikuwa nimeleweshwa na dawa. Nilikaa wiki mbili zaidi; hadi leo huenda sikumbuki baadhi ya mambo yalivyokuwa yanakwenda, lakini hali ilikuwa mbaya sana.
“Walisema nilikufa. Nilikuwa bado na hali ya kuleweshwa na dawa. Nilikuwa nimetulia kwenye koma kwa siku 18 na nilipozinduka sikujua ni siku gani.”