Kisa Israel, Uefa, FIFA vichwa vinauma
Muktasari:
- Kamati Kuu ya UEFA inatarajiwa kukutana wiki ijayo kuamua iwapo itaisimamisha Israel au la, huku ikielezwa wanachama wengi wanaunga mkono mpango wa kuifungia.
NYON, SWITZERLAND: UEFA na FIFA wako kwenye mtifuano mkubwa kuhusu uamuzi wa kuifungia Israel kushiriki Kombe la Dunia lijalo litakalopigwa Amerika ya Kaskazini.
Kamati Kuu ya UEFA inatarajiwa kukutana wiki ijayo kuamua iwapo itaisimamisha Israel au la, huku ikielezwa wanachama wengi wanaunga mkono mpango wa kuifungia.
Kikundi cha washauri wa Umoja wa Mataifa kimeitaka UEFA iifungie Israel, baada ya Tume ya Uchunguzi ya UN kubaini taifa hilo linatenda mauaji huko Gaza.
Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sanchez, pia ametoa wito wa kuwepo kwa vikwazo vya michezo dhidi ya Israel.
Hata hivyo, kwa kuwa michuano ya kufuzu Kombe la Dunia ipo chini ya mamlaka ya FIFA, shirikisho hilo la kimataifa la soka bado litakuwa na uwezo wa kubadilisha uamuzi wowote wa UEFA wa kuifungia Israel.
Kwa sasa Israel ipo nafasi ya tatu kwenye Kundi I, ikiwa na mechi mbili mkononi zinazoipa nafasi kubwa ya kufuzu Kombe la Dunia.
Timu hiyo inayonolewa na Kocha Ran Ben Shimon ina alama sawa na Italia iliyopo nafasi ya pili.
Kawaida kinara wa kundi hupata tiketi ya moja kwa moja, huku anayemaliza wa pili akipata nafasi ya kwenda kucheza mchujo.
Kufungiwa na UEFA kutamweka Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kwenye mazingira magumu, kutokana na uhusiano wake wa karibu na Marekani pamoja na Rais, Donald Trump.
Serikali ya Marekani imesisitiza itajaribu kusitisha jaribio lolote la kuizuia Israel kushiriki fainali za Kombe la Dunia katika majira yajayo ikiwa itafuzu.
Wiki iliyopita Infantino alisema ni vigumu kuyaadhibu mataifa yanayohusika kwenye migogoro ya kivita.
Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani alisema: "Tutafanya kila jitihada kusimamisha mpango na juhudi zozote za kujaribu kuifungia timu ya taifa ya Israel kushiriki Kombe la Dunia."
Iwapo UEFA itapiga kura kuiondoa Israel kwenye michuano ya Ulaya ya timu za taifa na klabu, itasababisha pambano la Europa League kati ya Aston Villa na Maccabi Haifa kufutwa.
Urusi imekuwa ikifungiwa kushiriki michuano ya Ulaya tangu kuivamia Ukraine mwaka 2022.
Vilevile Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) iliwawekea marufuku wanamichezo wa Urusi kucheza michezo mbalimbali ya mashindano hayo chini ya bendera ya taifa lao kama ilivyokuwa ya Paris mwaka 2024.