Gary Neville ashtushwa na taarifa za kuondoka kwa Guardiola
Muktasari:
- Manchester City tayari imetwaa mataji ya Kombe la Carabao na Kombe le FA msimu huu, na kufanya jumla ya mataji makubwa aliyoshinda Guardiola kufikia 20 katika kipindi cha muongo mmoja aliodumu klabuni hapo.
Habari za ghafla kuhusu kuondoka kwa kocha wa Manchester City, Pep Guardiola zimegonga vichwa vya habari na kumshtua mchambuzi wa soka Gary Neville, huku zikitokea katikati ya mchezo wa Arsenal dhidi ya Burnley.
Wakati Arsenal ikipambana uwanjani jana, taarifa za chinichini kutoka vyanzo vya kuaminika zinasema kuwa aliyekuwa kocha wa Chelsea na msaidizi wa zamani wa Guardiola, Enzo Maresca, anapewa nafasi kubwa ya kurithi mikoba hiyo msimu ujao.
Katika mchezo huo, Arsenal ilifanikiwa kupata ushindi mwembamba wa bao 1-0 na hivyo kuweka tofauti ya pointi tano mbele ya Manchester City.
Kai Havertz alikuwa shujaa wa mchezo huo kwa kufunga bao la ushindi, ingawa alinusurika kadi nyekundu baada ya kucheza rafu mbaya dhidi ya Lesley Ugochukwu.
Kutokana na matokeo hayo, Arsenal inaweza kutangazwa kuwa mabingwa leo usiku ikiwa Manchester City itashindwa kuifunga Bournemouth.
Mchambuzi na mchezaji wa zamani wa Man United, Gary Neville ameonyesha kushangazwa na namna habari hizo kubwa zilivyovuja wakati City ikiwa bado kwenye mapambano ya kuwania taji na ikiwa ni usiku wa kuamkia mechi yao muhimu.
"Nimeshtushwa sana kwamba jambo hili limevuja sasa hivi, hasa katikati ya mechi hii na usiku wa kuamkia mechi ya Man City. Kama ni kweli, uongozi wa Man City na Guardiola mwenyewe watakuwa wamekasirishwa sana na kuvuja kwa taarifa hizi sasa," amesema Neville.
Licha ya Arsenal kuwa na nafasi kubwa ya kubeba ‘ndoo’ ya Ligi Kuu ya England, Guardiola hataondoka mikono mitupu msimu huu.
Manchester City tayari imetwaa mataji ya Kombe la Carabao na Kombe le FA msimu huu, na kufanya jumla ya mataji makubwa aliyoshinda Guardiola kufikia 20 katika kipindi cha muongo mmoja aliodumu klabuni hapo.