Enzo Maresca kupokea kijiti cha Pep Guardiola Man City
Muktasari:
- Habari za kutoka SunSport zinaeleza kuwa Guardiola anapanga kuvunja mkataba wake uliosalia na kuondoka Etihad. Hatua hiyo imemfanya Maresca (46) kuwa chaguo namba moja na la muda mrefu klabuni hapo.
MANCHESTER, ENGLAND: Manchester City inajiandaa kumtangaza kocha wa zamani wa Chelsea, Enzo Maresca, kama mrithi wa Pep Guardiola ambaye anaripotiwa kufikia uamuzi wa kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu baada ya miaka 10 ya mafanikio makubwa.
Habari za kutoka SunSport zinaeleza kuwa Guardiola anapanga kuvunja mkataba wake uliosalia na kuondoka Etihad. Hatua hiyo imemfanya Maresca (46) kuwa chaguo namba moja na la muda mrefu klabuni hapo.
Maresca sio mgeni katika viunga vya Etihad. Alijiunga na klabu hiyo kwa mara ya kwanza mwaka 2020 kama kocha wa kikosi cha vijana na kufanikiwa kutwaa taji la Ligi mara mbili.
Baada ya kwenda Parma kwa muda mfupi, alirejea Manchester City Juni 2022 kama msaidizi mkuu wa Pep Guardiola. Alikuwa muhimili mkubwa katika benchi la ufundi lililoiwezesha City kutwaa Mataji Matatu ‘Treble’ msimu wa 2022-23.
Baada ya kuipandisha daraja Leicester City, Maresca alijiunga na Chelsea kwa mkataba wa miaka mitano. Licha ya kupata mafanikio makubwa katika msimu wake wa kwanza pale Stamford Bridge ikiwemo kutwaa mataji ya UEFA Conference League na Kombe la Dunia 2025, uhusiano wake na mabosi wa Chelsea uliingia mdudu.
Inaripotiwa kuwa Maresca alikiri mara tatu (mara mbili mwezi Oktoba na mara moja Desemba) kufanya mazungumzo ya siri na Manchester City ili kurithi mikoba ya Guardiola. Kitendo hicho cha ‘kuchepuka’ kiliwakasirisha viongozi wa Chelsea na kupelekea kuondoka kwake klabuni hapo mapema mwaka huu.
Wakati tetesi hizi zikishika kasi, Guardiola anakabiliwa na mechi mbili za mwisho za kukamilisha msimu wa EPL dhidi ya Bournemouth na Aston Villa. Kama Arsenal itateleza, Guardiola anaweza kuondoka Etihad akiwa ameweka rekodi ya kutwaa taji lake la saba la ligi kuu ya England, baada ya kunyakuwa mataji la Kombe la Ligi (Carabao) na Kombe la FA.
Alipoulizwa kuhusu matarajio yake baada ya ushindi wa Kombe la FA kwenye uwanja wa Wembley, Guardiola alijibu kwa mkato: "Tetesi? Uwe na usiku mwema," kabla ya kuondoka haraka.