Gary Neville ashangaa ujuzi wa Amorim
Muktasari:
- Amorim aliipa kisogo fomesheni ya 3-4-3 na kuhamia kwenye 4-2-3-1 alipoanza dhidi ya Newcastle, huku mfungaji wa bao pekee katika mechi hiyo, Patrick Dorgu alichezeshwa kwenye wingi ya kulia.
MANCHESTER, ENGLAND: GARY Neville amesema Ruben Amorim amechezesha kikosi cha ajabu sana cha Manchester United kuwahi kukiona wakati miamba hiyo ya Old Trafford ilipopambana kushinda 1-0 dhidi ya Newcastle United kwenye Boxing Day.
Amorim aliipa kisogo fomesheni ya 3-4-3 na kuhamia kwenye 4-2-3-1 alipoanza dhidi ya Newcastle, huku mfungaji wa bao pekee katika mechi hiyo, Patrick Dorgu alichezeshwa kwenye wingi ya kulia.
Diogo Dalot alicheza kwenye beki ya kulia, akipanda na kushuka, huku Luke Shaw akipangwa kwenye namba yake ambayo amekuwa akiimudu vyema, beki wa kushoto.
Ayden Heaven alicheza pacha na Lisandro Martinez kwenye beki ya kati, wakati Manuel Ugarte aliungana na Casemiro kwenye safu ya kiungo. Mason Mount na Cunha walikamilisha safu ya washambuliaji watatu sambamba na Dorgu, huku Benjamin Sesko akiongoza safu ya ushambuliaji.
Lakini, Casemiro alishangaa baada ya kutolewa kwenye kipindi cha pili akiingia beki Leny Yoro. Jack Fletcher, mtoto wa Darren naye alicheza kwenye mechi, akiwekwa kwenye kikosi sambamba na pacha wake, Tyler wakati alipoingizwa kipindi cha mapumziko kuchukua nafasi ya Mount, ambaye alipata maumivuw kwenye kipindi cha kwanza.
Joshua Zirkzee aliingizwa kuchukua nafasi ya Sesko na baadaye, Martinez na Shaw walitolewa na nafasi zao kuingizwa Tyler Fredricson na Tyrell Malacia, ambaye awali alikuwa hatakiwi na kocha Amorim na kumtaka aondoke kikosini.
Hiyo ina maana, Man United ilikuwa na mabeki sita wakati wanamaliza mechi hiyo na kufanikiwa kulinda pointi zao tatu.
Ugarte na Fletcher walicheza chini zaidi, wakati Zirkzee na Cunha walikuwa na kazi kubwa ya kukaba na kushambulia kiasi. Jambo hilo liliifanya Man United kumaliza mechi hiyo kwa kuchezesha fomesheni ambayo ilikuwa haieleweki ili kuwavuruga Newcastle United, jambo ambalo lilifanikiwa.
Gary Neville amesema: “Naweza kusema hiki ni kikosi cha ajabu cha Man United nilichowahi kukiona ambacho kilimaliza mechi hii. Lakini, waliweza kushikilia vyema. Walipambana kwa Newcastle walisukuma sana mashambulizi.”
Baada ya Man United kushinda, Neville amesema: “Kilikuwa kipindi cha pili balaa. Nadhani Man United ilikuwa kipindi cha kwanza. Nadhani walifanya vizuri sana, lakini kisha mabadiliko yakaanza kufanyika. Mtindo wa uchezaji ulibadilika, ikawa balaa. Kijana Ayden Heaven alikuwa vizuri sana. Aliokoa kila hatari na alipongezwa na Luke Shaw na benchi la ufundi.”
Amorim alibadilika na kuanza na mabeki wanne licha ya kuwahi kusema hata Papa asingeweza kumshawishi kuachana na 3-4-3 na alifanya hivyo ili kuwa na uwezo wa kutengeneza nafasi nyingi dhidi ya beki za Newcastle.