Gary Neville: Chelsea shida ni kuzuia
Muktasari:
- Neville ambaye aliwahi kucheza Manchester United kwa mafanikio, amesema Chelsea ilipoteza mechi yake dhidi ya Leeds United, Jumatano kwa mabao 3-1 kutokana na muendelezo wao wa kufanya makosa sana katika safu ya ulinzi.
LONDON, ENGLAND: MCHEZAJI wa zamani wa England, Gary Neville amekosoa vikali namna Chelsea inavyokaba hali inayosababisha iruhusu sana mabao.
Neville ambaye aliwahi kucheza Manchester United kwa mafanikio, amesema Chelsea ilipoteza mechi yake dhidi ya Leeds United, Jumatano kwa mabao 3-1 kutokana na muendelezo wao wa kufanya makosa sana katika safu ya ulinzi.
Katika mechi hiyo ambayo bao la tatu lilisababishwa na makosa binafsi ya mastaa Malo Gusto na Tosin Adarabioyo, Chelsea ilikuwa na matumaini ya kukusanya alama zaidi na kuzidi kuisogelea Arsenal katika msimamo wa ligi.
"Hili ni jinamizi linaendelea kumwandama Maresca, katika mechi ya leo, mabeki walikuwa wakiwapa sana moyo washambuliaji wa Leeds kutokana na makosa ambayo walikuwa wakiyafanya. Kiukweli mabeki wa kati wa timu hii wamekuwa wazembe, wanapenda sana kurudisha mipira katika eneo lao la boksi jambo ambalo ni hatari sana," amesema Neville.
Akiendelea kuzungumza kupitia Sky Sports, lejendi huyo amesema Chelsea kwa sasa ina kikosi cha kupenya kwenda nafasi za mbele katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini haina uwezo wa kushinda taji la Ligi Kuu England.
"Ninavyoona, Chelsea itamaliza nafasi ya nne au ya tano, shida mabeki wao wa kati wamekuwa wabovu, wanacheza taratibu, hawakabi vizuri. Kipa wao pia hana kiwango cha kuipa timu taji, na washambuliaji wao hawafijafikia ubora wa kuipa timu ubingwa."
Mfungaji wa Chelsea, Pedro Neto, aliyeingia kipindi cha pili na kufunga bao lao pekee, amesema baada ya kucheza vyema dhidi ya Arsenal Jumapili, waliona mechi dhidi ya Leeds ingeenda kuwa rahisi.
Chelsea sasa ina tofauti ya pointi tisa nyuma ya kinara Arsenal, ambayo ilifanikiwa kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Brentford siku hiyo hiyo.