Garathe Southgate hataki dili la Man United
Muktasari:
- Southgate, ambaye hana timu tangu aache kuifundisha timu ya taifa ya England, hii ni mara ya pili kuhusishwa na ajira ya Man United kwani awali aliripotiwa kuwa huenda angechukua mikoba ya Erik ten Hag lakini ilishindikana na yeye mwenyewe akaweka wazi kuwa asingeweza kuachana na timu ya taifa ya England kabla ya michuano ya Euro 2024.
MANCHESTER, ENGLAND: TAARIFA za ndani zinadai mabosi wa Manchester United wamepokea taarifa za kushangaza kuhusu kocha Gareth Southgate ambaye alikuwa katika mipango yao ya kwenda kuchukua kijiti kutoka kwa Ruben Amorim ambaye mambo yanaonekana kuwa mabaya kwake siku hadi siku.
Southgate, ambaye hana timu tangu aache kuifundisha timu ya taifa ya England, hii ni mara ya pili kuhusishwa na ajira ya Man United kwani awali aliripotiwa kuwa huenda angechukua mikoba ya Erik ten Hag lakini ilishindikana na yeye mwenyewe akaweka wazi kuwa asingeweza kuachana na timu ya taifa ya England kabla ya michuano ya Euro 2024.
Tangu ajiunge na Man United, Amorim ameshinda mechi 18 tu kati ya 49 na msimu uliopita alishindwa kuiwezesha timu hiyo kushiriki mashindano ya Ulaya na ikatolewa pia katika hatua ya awali ya Kombe la Ligi na Grimsby ya Ligi Daraja la Tatu.
Tovuti ya The Mirror imefichua kuwa Southgate amekataa ofa kutoka Manchester United kwani hana haraka ya kurejea kufundisha kwa sasa ingawa hajastaafu.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 55, kwa sasa muda mwingi anautumia na familia yake na anataka kukusanya nguvu kwanza na sio kuharakisha kurejea kazini.
Southgate ameendelea kuhudhuria mechi nyingi kubwa za soka, hasa EPL ikiwamo za Man United na ana urafiki wa karibu na aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo wa Man United, Dan Ashworth, ambaye alitajwa kutaka kumwajiri hapo awali.
Nyota wa zamani wa timu ya taifa ya England, Joe Cole ameishauri Man United kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inamwajiri Southgate akiamini ataisaidia.
Hata hivyo, licha ya kutopata matokeo mazuri, ripoti za hivi karibuni zinadai kuwa Amorim bado anaungwa mkono kikamilifu na bodi ya Man United na hawana mpango wa kumfukuza kwa sasa ingawa mambo yanaweza kubadilika ikiwa hali itaendelea kuwa mbaya.