FRMF yamrithisha Mohamed Ouahbi mikoba ya Walid Regragui
Muktasari:
- Uamuzi huu umekuja baada ya Regragui kujiuzulu kufuatia kufungwa na Senegal katika mechi ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) Januari 18, 2026.
SHIRIKISHO la Soka la Morocco (FRMF), limemtangaza Mohamed Ouahbi kuwa Kocha Mkuu mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo, akichukua nafasi ya Walid Regragui.
Uamuzi huu umekuja baada ya Regragui kujiuzulu kufuatia kufungwa na Senegal katika mechi ya fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) Januari 18, 2026.
Regragui, ambaye alikuwa ameahidi kuondoka ikiwa hatatwaa ubingwa huo, amehusishwa pia na mpango wa kujiunga na klabu ya Olympique de Marseille ya nchini Ufaransa.
Uteuzi wa Ouahbi unaonekana kama hatua ya kimkakati ya FRMF kuendeleza mfumo wa kukuza vijana. Ouahbi atasaidiwa na aliyekuwa msaidizi wa José Mourinho, João Sacramento, pamoja na mchezaji wa zamani wa Morocco, Youssouf Hadji.
Kocha huyo mzawa aliiwezesha timu ya taifa ya Morocco chini ya miaka 20 kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia la Vijana (U-20) mwaka 2025, akiifunga Argentina katika fainali.
Alifanya kazi kwa miaka 17 katika akademia ya RSC Anderlecht ya Ubelgiji akikuza nyota wengi wanaocheza soka la kulipwa Ulaya kwa sasa.
Ouahbi anamiliki leseni ya juu ya ukocha ya UEFA Pro na anajulikana kwa soka lenye nidhamu na mipango ya muda mrefu.
Ouahbi anaingia madarakani huku kukiwa na muda mchache kuelekea Kombe la Dunia 2026. Jukumu lake la kwanza litakuwa kurejesha utulivu kikosini, kusimamia mabadiliko ya wachezaji baada ya kustaafu kwa nahodha Romain Saïss, na kuhakikisha kasi ya mafanikio ya Morocco inaendelea katika ngazi ya wakubwa kama ilivyo katika timu za vijana.