Florian Wirtz mdomoni mwa timu vigogo Ulaya

Muktasari:
- Mabosi wa Man City wanataka kuweka ofa nono ili kuhakikisha wanamshawishi myota huyo kukataa ofa nyingine kutoka Real Madrid na Bayern Munich wanaohitaji huduma yake.
MANCHESTER City imeendelea kufanya mazungumzo na winga wa Bayer Leverkusen na Ujerumani, Florian Wirtz kwa ajili ya kumsajili katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Mabosi wa Man City wanataka kuweka ofa nono ili kuhakikisha wanamshawishi myota huyo kukataa ofa nyingine kutoka Real Madrid na Bayern Munich wanaohitaji huduma yake.
Awali, staa huyo alikuwa akiwindwa na timu mbalimbali Ulaya katika dirisha lililopita la majira ya kiangazi baada ya kuonyesha kiwango bora na kuisaidia Leverkusen kuchukua ubingwa.
Tangu kuanza kwa msimu huu Wirtz amecheza mechi 39 za michuano yote akifunga mabao 15 na kutoa asisti 13. Mkataba wake unamalizika 2027 na Leverkusen inahitaji kiasi kisichopungua Pauni 70 milioni ili kumuuza.
MANCHESTER City imepanga kuwasilisha ofa katika timu ya Crystal Palace ili kumsajili kiungo wa timu hiyo, Adam Wharton, 21 kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi Ulaya. Wharton amekuwa akihusishwa na Man City tangu dirisha la majira ya baridi mwaka jana ikielezwa kwamba kocha Pep Guardiola anamuona kama sehemu ya mipango yake ya muda mrefu.
CHELSEA na Barcelona zimeonyesha nia haswa ya kutaka kumsajili winga wa AC Milan na Ureno, Rafael Leao, 25, katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi, baada ya staa huyo kuonyesha nia ya kuondoka ikiwa AC Milan itashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. Tangu kuanza kwa msimu huu mchezaji huyo amecheza mechi 39 za michuano na kufunga mabao 10.
BEKI kisiki wa Everton na England, Jarrad Branthwaite huenda akawa mchezaji anayelipwa mshahara mkubwa zaidi katika timu hiyo ikiwa atasaini mkataba wa kuendelea kuichezea. Kwa mujibu wa taarifa, Branthwaite anahitaji mshahara wa Pauni 150,000 kwa wiki utakaokuwa mshahara mkubwa zaidi. Mkataba wa sasa wa nyota huyo unatarajiwa kumalizika 2027.
ARSENAL, Liverpool na Chelsea zipo kwenye vita kali ya kuwania saini ya mshambuliaji wa Inter Milan na Ufaransa, Marcus Thuram, 27, dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Licha ya kuonyesha nia ya kumsajili, Inter Milan imeanza mazungumzo na wawakilishi wa Thuram ili kumsainisha mkataba mpya. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika 2028.
KIUNGO wa Bayern Munich na Ujerumani, Joshua Kimmich, 30, amekubali kusaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia timu hiyo hadi ifikapo 2029. Awali nyota huyo alikuwa akihusishwa kuondoka mwisho wa msimu huu ambapo Arsenal na Manchester United zilikuwa zinahusishwa naye. Mkataba wa sasa wa Kimmich unamalizika mwisho wa msimu huu.
JUVENTUS inataka kutuma ofa PSG kwa ajili ya kuipata huduma ya mshambuliaji wa timu hiyo na Ufaransa, Randal Kolo Muani kwa mkopo wa msimu mmoja zaidi baada ya kufurahishwa na kiwango alichoonyesha tangu ajiunge nayo msimu huu. Mkataba wa Muani na PSG unatarajiwa kumalizika 2028 na sasa yupo Juventus.
BARCELONA imeanza mazungumzo na wawakilishi wa kipa wake raia wa Poland, Wojciech Szczesny, 34, kwa ajili ya kumsainisha mkataba mpya wa kuendelea kusalia kikosini. Mkataba wa sasa wa Szczesny unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu. Kipa huyo alisajiliwa Januari, mwaka huu kuziba nafasi ya Marc Andre ter Stegen ambaye alikumbwa na majeraha.