Everton yamkingia kifua Slot Liverpol
Muktasari:
- Kichwa cha beki Virgil van Dijk kinaweza kuwa ndicho kilichookoa kazi ya Slot katika ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Everton kwenye Dabi ya Merseyside iliyopigwa juzi na timu hiyo ilifufua mbio za kuisaka Top Four msimu huu ili ishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
LONDON, ENGLAND: USHINDI wa Liverpool wa mabao 2-1 dhidi ya Everton ugenini katika Ligi Kuu England unaelezwa umewagawa viongozi na maofisa wa juu wa klabu kuhusu mustakabali wa Kocha Arne Slot kuwapo au kuondoka katika kikosi hicho mwisho wa msimu.
Kichwa cha beki Virgil van Dijk kinaweza kuwa ndicho kilichookoa kazi ya Slot katika ushindi wa dakika za mwisho dhidi ya Everton kwenye Dabi ya Merseyside iliyopigwa juzi na timu hiyo ilifufua mbio za kuisaka Top Four msimu huu ili ishiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kwa sasa timu hiyo ina pointi tatu nyuma ya Manchester United katika msimamo - ikiwa nazo 55 huku Mashetani Wekundu wa Old Trafford wakishika nafasi ya tatu wakiwa na 58 sawa na Aston Villa inayoshika nafasi ya nne. Liverpool inakamata nafasi ya tano.
Beki huyo ambaye pia ni nahodha wa kikosi hicho pamoja na Uholanzi aliruka juu zaidi katika dakika ya 10 ya muda wa nyongeza wa kipindi cha pili na kufunga bao la ushindi kuipa Liverpool ushindi wa 2-1, matokeo yaliyoifanya Liverpool kubaki nafasi ya tano.
Muhimu zaidi, waliweka tofauti ya pointi saba dhidi ya Chelsea walio nafasi ya sita baada ya Chelsea kupoteza mechi yake nne mfululizo dhidi ya Manchester United, huku zikiwa zimebaki mechi tano kumalizika kwa ligi hiyo, ambapo matajiri wa klabu wanachotaka ni kufuzu tu mashindano hayo baada ya kikosi chao kuandamwa na majeruhi miezi ya karibuni na kuamua kujitoa katika mbio za ubingwa.
Kutokana na hali hiyo, taarifa kutoka ndani ya menejimenti ya klabu zinadai kufuzu Ligi ya Mabingwa kunaweza kumhakikishia Slot kubaki kazini kwani wakubwa watakuwa wameridhishwa na hatua hiyo ambayo wanaamini ni kubwa zaidi kwa sasa.
“Ulikuwa ushindi mkubwa. Nafasi ya Ligi ya Mabingwa ni muhimu sana kwa Liverpool. Kungekuwa na maswali kama wasingefanikiwa kufuzu, lakini bado hawajafika huko rasmi, hata hivyo inaaminika watafika,” kilisema chanzo kilicho karibu na mabosi wa klabu kilichodai wameridhishwa na matokeo ya wikiendi iliyopita.
Hata hivyo, Liverpool haikuwa bora katika mechi hiyo, kwani Everton walionyesha upinzani mkali na walikaribia kupata sare.
“Naam, baadhi ya mashabiki wa Liverpool wanaweza kuwa na wasiwasi kutokana na kiwango cha hivi karibuni. Lakini kwa upande wa Slot, ninaamini atapewa nafasi ya kujipanga upya kwa msimu ujao,” kilisisitiza chanzo hicho.
Iwapo Slot ataendelea kubaki Liverpool kuna uwezekano mkubwa klabu itamuwezesha kufanya usajili mkubwa ili kuboresha kikosi.
Inaelezwa Liverpool imeingia kwenye mbio za kumsajili kiungo wa Crystal Palace, Adam Wharton, ambaye thamani yake inakadiriwa kufikia Pauni 80 milioni.
Usajili huo unaweza kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa ya kiungo cha kati, huku hatma ya Curtis Jones na Alexis Mac Allister ikiwa haijulikani. Jones aliwahi kuhusishwa na uhamisho kwenda Inter Milan, wakati Mac Allister amekuwa na kiwango kisichoridhisha hivi karibuni. Iwapo Liverpool watamsajili Wharton, matumizi yatazidi Pauni 500 milioni katika misimu miwili iliyopita.
Timu hiyo pia ilivunja rekodi ya usajili wa England mara mbili majira ya joto yaliyopita kwa kuwasajili Alexander Isak na Florian Wirtz, ingawa bado hawajafikia matarajio makubwa yaliyotarajiwa kutokana na ada zao kuwa kubwa. Hata hivyo, baada ya msimu mmoja wa kuzoea mbinu za Slot, kuna matumaini kuwa mwendelezo wa kocha huyo unaweza kuleta mafanikio zaidi msimu ujao.