Slot asema Liverpool haitabadilisha mfumo wa usajili
Muktasari:
- Slot, 47, alikuwa katika presha kubwa baada ya kupoteza mechi nne kati ya saba zilizopita na ameshinda mbili tu.
LIVERPOOL, ENGLAND: KOCHA wa Liverpool, Arne Slot ametoa mwanga kuhusu mipango ya usajili ya dirisha lijalo la majira ya kiangazi, akisisitiza hana mpango wa kuondoka katika kikosi hicho.
Slot, 47, alikuwa katika presha kubwa baada ya kupoteza mechi nne kati ya saba zilizopita na ameshinda mbili tu.
Sehemu kubwa ya mashabiki wa Liverpool wanaonekana wakihitaji kocha huyo afutwe kazi mwishoni mwa msimu huu, lakini viongozi wa majogoo hao wanaonekana kuwa na mawazo tofauti.
Alhamisi ya wiki iliyopita, Andy Robertson alitangaza ataondoka katika viunga hivyo vya Anfield Juni mwaka huu, akifuata nyayo za Mohamed Salah ambaye pia amethibitisha kuondoka msimu utakapomalizika.
Wachezaji hao wawili, ni miongoni mwa mastaa wenye uzoefu mkubwa katika kikosi cha Slot na walikuwa sehemu muhimu ya mafanikio makubwa ya Liverpool kuanzia mwaka 2017.
Kuondoka kwao kutawaacha Wataru Endo, Alisson Becker, Virgil van Dijk na Joe Gomez kama wachezaji pekee wenye umri wa zaidi ya miaka 28 kwenye kikosi hicho.
Baadhi ya mashabiki wamekuwa wakitaka kikosi hicho cha Liverpool kusajili wachezaji waliokomaa zaidi katika dirisha lijalo tofauti na sera yao ya sasa ya kusajili mastaa wenye umri mdogo.
Hata hivyo, Slot amesema wamiliki wa klabu hiyo, Fenway Sports Group, hawatabadilisha mwelekeo wao.
“Mtindo wetu uko wazi kabisa. Haimaanishi kwamba hatuwezi kabisa wachezaji wenye umri mkubwa, tuliwahi kufanya hivyo kwa Endo na labda Federico Chiesa ambao walikuwa na umri wa juu kidogo, lakini sidhani kama klabu iliyofanikiwa kama tulivyo itabadilisha kabisa mfumo wake baada ya msimu mmoja ambao haukuwa mzuri sana. Kumekuwa na misimu mingi ambayo matokeo hayakuwa kama yalivyotarajiwa, lakini wameendelea kushikilia mfumo ule ule ambao unalenga wachezaji vijana wenye umri mdogo zaidi."