Everton 2 Man Utd 2: Refa ainyima penalti Everton jiooni
Muktasari:
- Man United ilionekana kutokuwa na jambo lolote kwenye kipindi cha kwanza na kukubali kipigo cha mabao 2-0 hadi kufikia mapumziko.
LIVERPOOL, ENGLAND: EVERTON imenyumwa penalti kwenye dakika za majeruhi wakati Manchester United ikipambana kutoka nyuma na kuambulia sare ya mabao 2-2 katika mchezo wa Ligi Kuu England uliofanyika uwanjani Goodison Park, leo Jumamosi.
Man United ilionekana kutokuwa na jambo lolote kwenye kipindi cha kwanza na kukubali kipigo cha mabao 2-0 hadi kufikia mapumziko.
Makosa kwenye safu ya ulinzi ya Man United yalimfanya Beto kuifungia Everton bao la kuongoza, ambalo lilihitaji dakika kadhaa za kuangaliwa kwenye VAR kabla ya kukubalika.
Abdoulaye Doucoure alifunga bao la pili kwa kichwa baada ya shambulizi la Jack Harrison kuokolewa na kipa Andre Onana na baada ya hapo Everton ilionekana kuwa tishio zaidi uwanjani.
Dakika chache baada ya kipindi cha pili kuanza, Doucoure alipata nafasi nyingine ya kufunga, lakini Onana aliokoa, huku Man United ikionekana kutokuwa na maajabu yoyote ya kupata matokeo kwenye mechi hiyo.
Lakini, kutoka kusikojulikana, Man United ilijikuta ikirudi mchezoni baada ya Bruno Fernandes kufunga kwa friikiki ambayo ilimpoteza kipa wa Everton, Jordan Pickford.
Man United ilisawazisha tena baada ya friikiki nyingine ya Fernandes kubabatiza mtu na mpira kumkuta Manuel Ugarte, aliyeutuliza vyema nje kidogo ya boksi na kufunga kwa shuti maridadi.
Lakini, kikosi hicho cha kocha Ruben Amorim nusura kipoteze pointi hiyo moja ya ugenini baada ya mwamuzi wa kati, Andy Madley kuonyesha kuwa ni penalti kutokana na Ashley Young kuangushwa ndani ya boksi.
Mwamuzi huyo alishauriwa kwenda kuangalia tukio hilo kwenye mashine ya VAR iliyokuwa uwanjani hapo na kubadilisha uamuzi wa awali kwa kufuta mkwaju huo wa penalti akidai kwamba Young alijiangusha kirahisi, hivyo haikuwa penalti na Man United ikafanikiwa kuondoka uwanjani hapo na pointi moja.
Matokeo hayo yanaifanya Man United kubaki kwenye nafasi ya 15 katika msimamo wa ligi hiyo ikiwa imekusanya pointi 30 katika mechi 26, huku Everton ikiwa nafasi ya 12 ikiw na pointi 31 katika mechi 26.