Evander Holyfield yamemkuta kama ya mpinzani wa Mwakinyo

Muktasari:

  • Ushindi wa Vítor Vieira Belfort ni wa pili kwenye ngumi baada ya ule wa Novemba 4, 2006 alipomchapa Josemario Neves    kwa KO, huku akiwa na rekodi ya mechi 41 kwenye mixed martial arts, ameshinda mara 26 (18 kwa KO, 3 kwa submission na 2 kwa decision, amepigwa mara 14 (7 kwa KO, 2 kwa submission na 5 kwa decision.

Evander Holyfield nguli wa zamani wa dunia wa uzani wa juu, usiku wa kuamkia leo amepigwa kwa Technical Knock Out (TKO) raundi ya kwanza kwenye jimbo la Florida, Marekani.

Kipigo hicho ni kama kilichowahi kumkuta Julius Indongo bondia aliyecheza na Hassan Mwakinyo hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kuokolewa na mwamuzi John Chagu.

Holyfield au The Real Deal kama anavyopenda kujiita aliokolewa na mwamuzi  mbele ya Mbrazili, Vitor Belfort mwanamichezo wa mixed martial arts ambaye amezidiwa miaka 14 na Holyfield mwenye miaka 58.

Katika pambano hilo, Evander alishambuliwa mfululizo bila majibu akiwa amebananishwa kwenye kona kabla ya refarii kumuokoa na kuonyesha ishara ya kumaliza pambano huku mpinzani wake ambaye hilo ni pambano lake la pili la ndondi kutangazwa mshindi.

Video ya pambano hilo inamuonyesha Holyfield akionyesha kana kwamba hakufurahishwa na uamuzi wa refarii, ingawa kabla ya kushambuliwa mfululizo alidondoshwa chini na konde la mpinzani wake ambaye ni mkali zaidi wa michezo mchanganyiko kama ngumi, mchezo wa asili wa Kibrazil wa jiu-jitsu, Muay Thai, Judo na Shotokan.

Hilo ni pambano la kwanza kwa Holyfield tangu lile la Mei 7, 2011 alipomchapa kwa TKO, Brian Nielsen na kufunga rekodi ya kucheza mapambano 56 yaliyoingizwa kwenye rekodi za mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia (boxrec).

Hadi anastaafu, Holyfield alikuwa na rekodi ya kupigwa kwa Knock Out na mabondia wawili pekee, James Toney mwaka 2003 na Riddick Bowe mwaka 1995, kipigo cha leo alfajiri pamoja na kwamba hakijawekwa kwenye Boxrec lakini ni cha tatu kwa bondia huyo kuchapwa kwa TKO.

Mapambano mengine manane alipigwa kwa pointi likiwamo lile la Lennox Lewis, huku katika mapambano 44 aliyowahi kushinda, 29 ilikuwa ni kwa KO likiwamo lile la Mike Tyson la mwaka 1996 aliposhindwa kwa TKO.

Mwaka mmoja baadae walirudiana June 28 na Holyfield kuendeleza rekodi ya ushindi kwa matokeo ya DQ baada ya Tyson kuondolewa mchezoni kwenye pambano lililokuwa la raundi 12.