Eti kocha Arteta hatoboi Krismasi

Muktasari:
- KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ametabiriwa atafutwa kazi Krismasi ya mwaka huu.
LONDON, ENGLAND: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta ametabiriwa atafutwa kazi Krismasi ya mwaka huu.
Hiyo ni kwa mujibu wa gwiji wa klabu hiyo, Paul Merson, ambaye alisema kitu ambacho kitamwokoa kocha huyo asionyeshwe mlango wa kutokea msimu ujao itakapofika Krismasi kama tu Arsnal itakuwa kwenye nafasi ya pili au vinara kwenye msimamo wa Ligi Kuu England.
Kinyume cha hilo ni mabosi wa Arsenal wataingia sokoni kusaka kocha mpya kama timu hiyo haitakuwa kwenye nafasi mbili za juu kabla ya Mwaka Mpya kuingia.
Arsenal imemaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu England ikiwa ni msimu wa tatu mfululizo, huku wengi wakiamini Arteta 43, atakuwa na kibarua kizito msimu ujao kwa sababu ndiyo utakaobeba hatima ya ajira yake kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Arsenal haijashinda taji lolote la Ligi Kuu England tangu 2004 na maswali yameshaanza kuibuka kama Mhispaniola huyo ana uwezo wa kutosha wa kuifanya timu hiyo kubeba taji.
Hilo limepata nguvu zaidi baada ya uamuzi wake wa kupuuzia usajili wa straika wa kiwango cha dunia, kitu ambacho kinaweza kuboreshwa kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi kutokana na kuwafukuzia mastraika kadhaa, akiwamo Viktor Gyokeres wa Sporting Lisbon na Benjamin Sesko wa RB Leipzig.
Lakini, gwiji Merson anaamini Arteta atakuwa na kazi ngumu kutoka sasa hadi Krismasi kutambua hatima ya ajira yake kwa maana ya kuifanya Arsenal kuwa ya kibabe Ligi Kuu England kinyume cha hapo, kibuti kitamhusu, kwa sababu hakutakuwa na kisingizio.
Merson alisema: “Huo ndiyo wasiwasi wangu. Nadhani Arteta ana muda kutoka sasa hadi Krismasi. Arsenal itahitaji kuwa kwenye nafasi mbili za juu hadi kufikia Krismasi ili abaki.
“Kama umeongoza timu kwa misimu zaidi ya minne bila ya taji, huwezi kuachwa uendelee. Unapopewa muda unapaswa uonyeshe. Unahitaji kushinda mataji.”