Enrique agomea mkataba mpya PSG
Muktasari:
- Kuna klabu kadhaa za Ligi Kuu England zimekuwa zikihusishwa na kocha huyo ambaye aliipa PSG ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
PARIS, UFARANSA: KOCHA, Luis Enrique ameripotiwa kwamba ataachana na Paris Saint-Germain mwishoni mwa msimu huu baada ya kupuuzia kusaini mkataba mpya.
Kuna klabu kadhaa za Ligi Kuu England zimekuwa zikihusishwa na kocha huyo ambaye aliipa PSG ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita.
Na mabosi wa PSG walimtarajia Enrique kutulizana kwenye klabu hiyo na kusaini mkataba mpya wa muda mrefu.
Mkataba wake wa sasa utafika tamati majira ya kiangazi yajayo. Lakini, Mhispaniola huyo mwenye umri wa miaka 55 ameiweka kwenye wakati mgumu timu yake baada ya kuripotiwa kupuuzia mpango wa kusaini dili jipya.
Marca linaripoti kwamba Enrique anadhani amefikia mafanikio makubwa anayotaka huko Paris. Na sasa kocha huyo wa zamani wa Barcelona anataka kwenda kukabiliana na changamoto mpya.
Na hilo linamfanya Enrique kuwa na machaguo kadhaa ya kwenda kupata kazi kwenye Ligi Kuu England. Novemba mwaka jana iliripotiwa, Liverpool ni moja ya timu zinazovutiwa na kocha huyo. Na hilo linakuja wakati kocha wa sasa Arne Slot akionekana kuishiwa mbinu za kuiongoza timu kufikia makali yao ya msimu uliopita, ambapo walinyakua ubingwa wa Ligi Kuu England.
Liverpool ilimweka kocha wao wa zamani Jurgen Klopp kwenye mipango ya kumrudisha kikosini endapo kama itamfuta kazi Slot. Lakini, kama hilo litafanyika, basi miamba hiyo ya Anfield itamhitaji Klopp kwa muda tu ili ikifika mwisho wa msimu wamchukue jumla Enrique.
Wakati huo huo, Manchester United itakuwa sokoni kutafuta kocha mpya baada ya kumfuta kazi Ruben Amorim.
Ole Gunnar Solskjaer na Michael Carrick kwa sasa wanatazamiwa kama wanaweza kwenda kuwa makocha wa muda huko Old Trafford hadi mwisho wa msimu. Na hilo linaweza kumtoa nafasi kwa Enrique kwenda kujaribu bahati yake Theatre of Dreams.
Mhispaniola huyo alijiunga na PSG mwaka 2023 na tangu wakati huo amewapata mataji mawili ya ubingwa wa ligi, mawili ya Kombe la Ufaransa na taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.