PSG yabanwa ugenini, Ajax ikipata ushindi wa kwanza UEFA
Muktasari:
- Kikosi hicho cha Luis Enrique kiko nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa, ingawa kipo tofauti ya pointi moja tu juu ya nafasi za juu nane, huku Athletic ikiwa nafasi ya 28 katika hatari ya kutolewa mashindanoni.
BILBAO, HISPANIA: Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris St-Germain (PSG) wameshindwa kuifunga Athletic Club licha ya kutawala mchezo. Hata hivuo, bado wana nafasi nzuri ya kusonga mbele hatua ya 16 bora.
Kikosi hicho cha Luis Enrique kiko nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi ya Mabingwa, ingawa kipo tofauti ya pointi moja tu juu ya nafasi za juu nane, huku Athletic ikiwa nafasi ya 28 katika hatari ya kutolewa mashindanoni.
PSG ilitawala mechi hiyo iliyochezwa usiku wa Desemba 10, 2025 kwenye Dimba la San Mames na ilipata nafasi nyingi za wazi, lakini haikupata njia ya kumfunga kipa wa wenyeji, Unai Simon.
Fabian Ruiz alipoteza nafasi mbili nzuri kwa kupiga juu ya lango, huku Simon akifanya kazi nzuri kumzuia Senny Mayulu kabla na baada ya kipindi cha pili.
Nafasi bora zaidi ya PSG ilikuja wakati Bradley Barcola alipokimbia moja kwa moja kuelekea golini na kupiga shuti kali lililogonga mwamba.
Ruiz pia alikaribia kuipatia PSG ushindi dakika za mwisho lakini shuti lake likaokolewa vyema na Simon, kisha Yuri Berchiche akazuia mpira katika mstari wa goli.
Wenyeji Bilbao, ambao walipata shuti lao la kwanza kulenga lango mwishoni kupitia Asier Hierro, wako pointi mbili tu nyuma ya nafasi ya kufuzu mtoano.
AJAX YAPATA USHINDI WA KWANZA
Katika Dimba la Tofig Bahramov Republican lililopo Baku nchini Azerbaijan, Ajax imepata ushindi wa kwanza kwenye kampeni ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu baada ya kutoka nyuma mara mbili na kuichapa Qarabag.
Mabingwa hao wa Ulaya mara nne, walikuwa wamepoteza mechi zao tano za kwanza kwenye mashindano hayo msimu huu, na walionekana kuelekea kupoteza ya sita walipokuwa wakiongozwa 2-1 hadi dakika ya 79, kabla ya Oscar Gloukh kupiga shuti kali kutoka yadi 20 na kusawazisha kuwa 2-2.
Dakika tatu baadaye, Anton Gaaei alipiga shuti zuri la kwanza kwa nguvu na kuwapa Ajax uongozi, huku ushindi ukikamilishwa na Gloukh tena aliyefunga kwa mpira wa chini uliotinga kona ya goli dakika ya 90.
Ushindi huo umeiondoa Ajax mkiani mwa msimamo wa timu 36, na sasa inakwenda kuikabili Villarreal Januari 20, 2026 kabla ya kumaliza hatua ya makundi nyumbani dhidi ya Olympiacos, Januari 28, 2026.
Hata hivyo, nafasi yao ya kumaliza ndani ya timu 24 za juu ili kuendelea na mashindano Februari 2026 inaonekana kuwa ndogo, kwani inaweza kufikisha alama tisa pekee, huku alama 11 ndizo zilizohitajika msimu uliopita.
Msimu huu mgumu kwa Ajax umeshuhudia vichapo vizito vya 4-0, 5-1 na 3-0 dhidi ya Marseille, Chelsea na Galatasaray mtawalia.
Katika hali ya mvua kubwa mjini Baku, Qarabag ilitangulia kupata bao dakika ya 10 kupitia Camilo Duran aliyelobisa mpira juu ya kipa Vitezslav Jaros aliyekuwa akitoka golini.
Kasper Dolberg alisawazisha dakika sita kabla ya mapumziko kwa shuti kali kutoka yadi 25, lakini Matheus Silva aliirejesha Qarabag mbele mara tu baada ya kuanza kipindi cha pili kwa shuti la chini lililoguswa na beki.
Qarabag, ambao hawajawahi kufika hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa, wana pointi saba kutokana na mechi sita. Watakuwa wenyeji wa Eintracht Frankfurt, Januari 21, 2026, kabla ya kusafiri kwenda Anfield kumenyana na Liverpool wiki moja baadaye.
MATOKEO YOTE UEFA OKTOBA 10, 2025
Villarreal 2-3 Copenhagen
Qarabağ 2-4 Ajax
Bayer Leverkusen 2-2 Newcastle
Dortmund 2-2 Bodø/Glimt
Benfica 2-0 Napoli
Juventus 2-0 Pafos
Athletic Club 0-0 PSG
Club Brugge 0-3 Arsenal
Real Madrid 1-2 Man City