ENGLAND: Guardiola ataka kufundisha England baada ya Bayern
Kocha kijana, Pep Guardiola.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
“Guardiola anasema, ‘Mimi ni mtu wa Barca na siku zote nitakuwa hivyo’ lakini hilo halimaanishi kwamba atarudi kuifundisha Barcelona. Kwa kweli kama mimi ningekuwa mcheza kamari basi ningesema baada ya hapa Bayern Munich atakwenda England,” alisema Perarnau.
MAISHA bado yapo kasi kwa kocha kijana, Pep Guardiola. Sasa ameziweka mkao wa kula klabu za Manchester City na Arsenal baada ya kutamka wazi kuwa ‘Nitakuja England’.
Mtu wa karibu wa Guardiola amefichua kwamba anatazamia kuwa kazi yake inayofuata itakuwa England na kauli hiyo itazua vita kwa klabu mbalimbali kubwa za England ambazo zitapenda huduma yake.
Kwa sasa Guardiola ana mkataba na Bayern Munich mpaka mwaka 2016 akiwa anatokea Barcelona ambapo alijijengea jina kubwa kwa kutwaa mataji mawili ya ubingwa wa Ulaya, mataji matatu ya La Liga, mawili ya Kombe la Mfalme, mawili ya Super Cup, na mawili ya Klabu Bingwa ya Dunia.
Manchester City inapewa nafasi kubwa ya kumchukua Guardiola kutokana na urafiki wake mkubwa na mkurugenzi wa ufundi wa timu hiyo, Txiki Begiristain, ambaye alicheza naye Barcelona na pia aliwahi kushika nafasi hiyo ya ukurugenzi wa ufundi Barcelona wakati Guardiola akiwa kocha.
Hata hivyo, kwa uamuzi wake wa kutaka kwenda England utaiweka Arsenal katika tahadhari wakati huu bosi mtendaji wa timu hiyo, Ivan Gatzidis akikiri kwamba kunahitajika umakini mkubwa kumpata kocha mbadala kuchukua nafasi ya Arsene Wenger mwenye umri wa miaka 65.
Mwandishi Marti Perarnau ambaye alizunguka mwaka mzima na Guardiola kwa ajili ya kuandika kitabu cha msimu wake wa kwanza akiwa na Bayern Munich ametoboa siri hiyo kwa kuandika maneno ya Guardiola yanayoashiria kuwa anataka kufundisha timu moja ya England.
“Guardiola anasema, ‘Mimi ni mtu wa Barca na siku zote nitakuwa hivyo’ lakini hilo halimaanishi kwamba atarudi kuifundisha Barcelona. Kwa kweli kama mimi ningekuwa mcheza kamari basi ningesema baada ya hapa Bayern Munich atakwenda England,” alisema Perarnau.
“Nani anajua? Anaweza kumaliza miaka yake minane au kumi ya mwisho akifundisha timu ya taifa. Hajapanga kufundisha soka kwa muda mrefu sana na inaonekana ana makubaliano hayo na familia”
“Labda atafanya hivyo siku moja, ingawa haitatokea haraka. Bado ana miaka mitatu Bayern Munich, na kama hataongeza mkataba wake basi sehemu atakayokwenda ni England,” alimalizia rafiki huyo.