Emiliano Martinez katua anga za Inter Milan
Muktasari:
- Hata hivyo, dili hilo lina kikwazo kikubwa kwani Martinez atalazimika kukubali kupunguziwa mshahara ikiwa atahitaji kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Italia.
INTER Milan inafikiria uwezekano wa kumsajili kipa wa Aston Villa na timu ya taifa ya Argentina, Emiliano Martinez, 33, katika dirisha la usajili wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo, dili hilo lina kikwazo kikubwa kwani Martinez atalazimika kukubali kupunguziwa mshahara ikiwa atahitaji kujiunga na mabingwa hao wa zamani wa Italia.
Inter Milan inataka kufanya maboresho katika nafasi ya kipa na kigezo chake kwa kipa inayemtaka ni mwenye uzoefu mkubwa wa michuano ya kimataifa kama ilivyo kwa Emiliano ambaye amewahi kushinda Kombe la Dunia akiwa na Argentina.
Martinez, aliyekuwa shujaa wa Argentina kwenye Kombe la Dunia 2022, bado ana mchango mkubwa Villa, lakini tangu msimu uliopita amekuwa akihusishwa kuondoka. Taarifa za ndani zinadai staa huyo alitaka kuondoka tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi, lakini ilishindikana kutokana na kiasi cha pesa ambacho Aston Villa ilitaka.Mkataba unamalizika 2029.
Jean-Philippe Mateta
ASTON VILLA imejitosa kumsajili mshambuliaji wa Crystal Palace na timu ya taifa ya Ufaransa, Jean-Philippe Mateta, 28, ambaye amekuwa akidaiwa kuwa anaweza akatimkia Juventus. Mabosi wa Palace tayari wameshaanza kujiandaa na maisha bila staa huyo na sasa wapo katika mazungumzo na mshambuliaji wa Aston Villa na Ivory Coast, Evann Guessand, 24, jambo linaloonyesha kuwa yanaweza kufanyika mabadilishano ya wachezaji.
Marcos Senesi
BOURNEMOUTH imeweka msimamo wa kutomuuza beki tegemeo, Marcos Senesi, 28, katika dirisha hili la usajili, licha ya Chelsea, Juventus na Barcelona kumuingiza beki huyo wa kimataifa wa Argentina katika orodha ya wachezaji zinaotaka kuwasajili. Bournemouth imepanga kuzuia ofa zitakazowasilishwa ikiamini Senesi ni mhimili muhimu wa safu ya ulinzi katika mbio za kusalia Ligi Kuu England. Msimamo huo unaashiria kuwa klabu hizo huenda zikasubiri mwisho wa msimu.
Troy Parrott
FULHAM ipo kwenye vita ya kuwania saini ya mshambuliaji wa kimataifa wa Ireland, Troy Parrott, 23, anayeichezea AZ Alkmaar ya Uholanzi.Hata hivyo, inakutana na ushindani kutoka Wolfsburg ya Ujerumani na Real Betis ya Hispania ambazo pia zimeonyesha nia ya kumsajili staa huyo katika dirisha la majira ya kiangazi. Parrott ameendelea kuonyesha kiwango bora Ligi Kuu Uholanzi na msimu huu amefunga mabao 19.
Leon Bailey
MKATABA wa mkopo wa winga wa Jamaica, Leon Bailey, 28, ndani ya Roma umesitishwa mapema kuliko ilivyotarajiwa baada ya klabu hiyo ya Italia kuamua kumrudisha Aston Villa. Bailey alikuwa hajafanikiwa kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha Roma, jambo lililosababisha pande mbili kukubaliana kusitisha mkopo mapema. Villa inadaiwa kutaka kumpeleka kwa mkopo mwingine huko Hispania
Noah Sadiki
SUNDERLAND imedai kuwa haina mpango wa kumuachia kiungo raia wa DR Congo, Noah Sadiki, 21, kwenda Manchester United au klabu nyingine yoyote katika dirisha hili la usajili. Sadiki amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika kikosi cha Sunderland kutokana na uwezo wake wa kucheza kama kiungo wa ulinzi, na pia beki wa pembeni na kiwango chake kimezivutia timu mbalimbali barani Ulaya.
Wilson Isidor
EVERTON imeanza mawasiliano na Sunderland kwa ajili ya kuulizia uwezekano wa kumpata mshambuliaji wa timu hiyo, Mfaransa Wilson Isidor, 25, katika dirisha lijalo la usajili ikiwa ni kwenye jitihada za kuimarisha safu ya ushambuliaji. Isidor ameonyesha uwezo mkubwa msimu huu na bado haijafahamika kama Sunderland iko tayari kumuuza kwa sasa. Mkataba wake unaisha 2028.
Yisa Alao
CHELSEA inadaiwa kuwa ipo hatua za mwisho kukamilisha dili la kumsajili beki kinda wa Sheffield Wednesday, Yisa Alao, 17, katika dirisha hili. Alao aliyejizolea sifa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kusoma mchezo licha ya umri mdogo, anatajwa kuwa atacheza nusu msimu timu za vijana kabla ya kupandishwa. Usajili wake ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu Chelsea ya kuongeza ushindani.