Eden ataja mchezaji bora aliyecheza naye
Muktasari:
- Winga huyo mwenye kipaji kikubwa anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kucheza katika Uwanja wa Stamford Bridge na bado anapendwa sana na mashabiki wa Chelsea duniani kote licha ya upendo wake kwa Real Madrid.
LONDON, ENGLAND: NGULI wa Chelsea, Eden Hazard, amewashangaza wengi baada ya kuwapuuza baadhi ya mastaa wakubwa wa zamani wa klabu hiyo alipomtaja mchezaji bora zaidi waliyewahi kucheza.
Winga huyo mwenye kipaji kikubwa anachukuliwa kuwa mmoja wa wachezaji bora kuwahi kucheza katika Uwanja wa Stamford Bridge na bado anapendwa sana na mashabiki wa Chelsea duniani kote licha ya upendo wake kwa Real Madrid.
Katika kipindi chake akiwa Chelsea, Hazard alicheza pamoja na karibu nyota wote wakubwa wa kihistoria wa klabu hiyo. Alijiunga na Chelsea majira ya joto ya mwaka 2012 na kukaa kwa miaka saba katika eneo la SW6, ambapo alifikia kiwango chake bora kuelekea mwisho wa kipindi chake klabuni hapo pamoja na wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Russia akiwa na timu ya taifa ya Ubelgiji.
Alishiriki uwanjani na nyota kama Frank Lampard, John Terry na Didier Drogba, ingawa wachezaji hao walikuwa tayari karibu na mwisho wa ubora wao alipowasili Chelsea. Hazard pia alicheza na N’Golo Kanté akiwa katika kiwango chake bora pamoja na mshambuliaji Diego Costa.
Hata hivyo, hakuna hata mmoja kati ya hao aliyechaguliwa na Hazard kuwa mchezaji bora zaidi aliyewahi kucheza naye. Pia hakuwataja wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya Ubelgiji, Kevin De Bruyne au Romelu Lukaku, ambao wote alikuwa na maelewano mazuri nao uwanjani. Hata mshindi wa Ballon d’Or, Luka Modric, hakuchaguliwa kuwa namba moja, licha ya Hazard kumaliza nafasi ya nane katika tuzo hiyo wakati Modric alipoishinda. Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe, Hazard alikuwa na mtu mmoja tu akilini mwake kwa nafasi ya kwanza, ambapo winga huyo alisema: “Kumekuwa na wachezaji wengi wazuri kati ya Chelsea na Real Madrid. Mshindi wa Ballon d’Or kama Luka Modric ni mchezaji mzuri sana. Frank Lampard, Didier Drogba au Samuel Eto’o kuelekea mwisho wa kipindi chake Chelsea. Lakini, kama ningelazimika kuchagua mmoja, ningemchagua Karim. Mshindi mwingine wa Ballon d’Or ambaye nilipata nafasi ya kucheza naye Real Madrid. Katika mechi na hata mazoezini alikuwa bora sana. Ningekuwa uwanjani naye na kusema, ‘Wow!’ Alikuwa ni sanaa halisi ya mpira wa miguu.” Mchezaji huyo aliyemtaja ni mshambuliaji wa zamani wa Real Madrid, Karim Benzema.