Eddie Howe kulamba mkwanja mrefu

Muktasari:
- Howe, 47, alimaliza ukame wa miaka 56 wa kubeba taji baada ya kuiongoza Newcastle kushinda 2-1 dhidi ya Liverpool, Jumapili kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi uliofanyika uwanjani Wembley.
NEWCASTLE, ENGLAND: KOCHA Eddie Howe anajiandaa kupata ongezeko la asilimia 50 la mshahara wake endapo kama Newcastle United itakamatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kushinda taji la Kombe la Ligi.
Howe, 47, alimaliza ukame wa miaka 56 wa kubeba taji baada ya kuiongoza Newcastle kushinda 2-1 dhidi ya Liverpool, Jumapili kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Ligi uliofanyika uwanjani Wembley.
Amekuwa Mwingereza wa kwanza tangu Harry Redknapp alipobeba taji la ndani mwaka 2008 na jambo hilo limemfanya ajizolee umaarufu mkubwa kwenye kikosi hicho cha St James’ Park.

Kwa Howe kushinda Kombe la Ligi ilikuwa ni ziada tu, lakini lengo kubwa la kwanza ilikuwa kumaliza Top Four ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Na kama hilo litatimia basi mshahara wake kwa mwaka utapanda hadi Pauni 9 milioni ikiwa ni bonasi atakazolipwa kutokana na makubaliano yaliyowekwa kwenye mkataba wake utakaofika ukomo 2028.
Mafanikio hayo yatalifanya jina lake kuzidi kushamiri kwenye orodha ya wanaopigiwa hesabu za kupewa timu ya taifa ya England. Howe alikuwa kwenye orodha hiyo wakati Gareth Southgate alipoachana na Three Lions kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana.

Lakini, kibarua hicho cha kuinoa England kwa sasa kipo chini ya Mjerumani Thomas Tuchel, ambaye atakuwa na majukumu ya kuingoza timu hiyo hadi wakati wa fainali za Kombe la Dunia 2026.