Dusan Vlahovic ni Spurs au Chelsea
Muktasari:
- Vlahovic, ambaye alijiunga na Juventus kutokea Fiorentina mwaka 2022 kwa ada ya takribani Euro 80 milioni, amekuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kwenye Serie A, lakini anataka kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
MSHAMBULIAJI wa Juventus, Dusan Vlahovic, 25, anataka kutua katika Ligi Kuu England kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi na timu pekee ambazo ameonyesha nia za kutaka kuvaa jezi zao ni Chelsea na Tottenham Hotspur.
Vlahovic, ambaye alijiunga na Juventus kutokea Fiorentina mwaka 2022 kwa ada ya takribani Euro 80 milioni, amekuwa mmoja wa washambuliaji hatari zaidi kwenye Serie A, lakini anataka kupata changamoto mpya sehemu nyingine.
Juventus ilikuwa ikitamani kumuuza kabla ya msimu huu kuanza lakini ilishindikana na inaweza kujaribu tena Januari kwa sababu akiondoka mwisho wa msimu haitopata kitu kwani mkataba wake utakuwa umemalizika.
Tangu kuanza kwa msimu huu, Vlahovic amefunga mabao sita na kutoa asisti moja katika mechi 11 za michuano yote.
Chelsea inamwona Vlahovic kama mrithi wa muda mrefu wa Nicolas Jackson, huku Tottenham ikimtazama kama mchezaji atakayechukua nafasi ya Harry Kane ambaye licha ya kuondoka tangu mwaka 2023 hadi sasa bado inapata tabu kuziba pengo lake.
Bruno Fernandes
KAPTENI wa Manchester United, Bruno Fernandes, mwenye umri wa miaka 31, hana mpango wa kuondoka katika timu hiyo kwenye dirisha lijalo la majira ya baridi, licha ya kupokea ofa kubwa kutoka Saudi Arabia. Kwa mujibu wa taarifa kutoka tovuti ya Talksport, klabu kadhaa vya Saudia zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili staa huyo kwa dau linalofikia Euro 80 milioni. Bruno amekataa na kusisitza kuwa anataka kumaliza msimu huu akiwa na Man United na baada ya hapo anaweza kufikiria kuondoka.
Harry Maguire
MAZUNGUMZO baina ya wawakilishi wa beki wa Manchester United, Harry Maguire na wawakilishi wa timu hiyo kuhusu mkataba mpya yameanza rasmi.Maguire ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, kwa mujibu wa The Sun, kocha Ruben Amorim amevutiwa sana na kiwango chake kiasi cha kuagiza apewe mkataba mpya ingawa utakuwa na punguzo la mshahara kutoka ule ambao anaupata kwa sasa.
Bernardo Silva
KIUNGO wa Manchester City, Bernardo Silva, 31, anatarajiwa kuondoka katika klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu ambapo tovuti ya GiveMeSport inaeleza kuwa klabu za Saudi Arabia na timu yake ya zamani, Benfica zinafanya mazungumzo na wawakilishi wake.Silva ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, amekuwa kiungo tegemeo katika kikosi cha Man City chini ya Pep Guardiola tangu 2017.
Tyrique George
CHELSEA imeweka wazi kuwa ipo tayari kusikiliza ofa kutoka timu zinazohitaji huduma ya mshambuliaji wake wa kimataifa wa England, Tyrique George, 19, mwenye umri wa miaka 19, katika dirisha lijalo la usajili wa majira ya baridi. Tyrique George ambaye amelelewa katika akademi ya Chelsea, anaonekana kuwa na kipaji kikubwa, lakini imekuwa ngumu kupata nafasi kikosini, hivyo ameomba kuuzwa au kutolewa kwa mkopo.
Endrick
WEST Ham United, Real Sociedad na Valencia zipo katika vita ya kuiwania saini ya kinda wa kimataifa wa Brazil, Endrick, 19, kutoka Real Madrid kwa mkopo katika dirisha lijalo. Ripoti kutoka tovuti ya Estadio Deportivo zinaelezwa, Endrick aliyetua Madrid mwaka 2024 akitokea Palmeiras anataka kuondoka kwa sababu amechoshwa na kukaa benchi, hivyo anataka atue timu itakayomchezesha.
Richarlison
ORLANDO City SC inayoshiriki Ligi Kuu ya Marekani inataka kumsajili mshambuliaji wa Tottenham Hotspur, Richarlison, 28, katika dirisha kubwa la usajili wa majira ya kiangazi mwakani. Inaelezwa Orlando tayari imeanza mazungumzo ya awali na wawakilishi wa Richarlison kuhusu uwezekano wa uhamisho huo, ambao utakuwa sehemu ya maboresho yanayoendelea.
Antoine Semenyo
MANCHESTER United imepiga hatua kubwa katika harakati za kumsajili mshambuliaji wa Bournemoth na timu ya taifa ya Ghana, Antoine Semenyo, 25, ambaye pia anawindwa na Liverpool. Semenyo amekuwa katika kiwango bora tangu kuanza kwa msimu wa 2025/26, akiwa amefunga mabao 5 na kutoa pasi 3 za mabao katika mechi za michuano yote.