Duh! Hii ya Bundesliga ni kali
Muktasari:
- Hilo limekuja baada ya mechi hiyo ilimalizika kwa matukio yenye utata mwezi uliopita.
BERLIN, UJERUMANI: VFL BOCHUM sare yao ya bao 1-1 dhidi ya Union Berlin imegeuka na kupewa ushindi wa mabao 2-0 na mabosi wa Bundesliga.
Hilo limekuja baada ya mechi hiyo ilimalizika kwa matukio yenye utata mwezi uliopita.
Bochum ilibaki na wachezaji 10 uwanjani kwenye dakika ya 13 tu baada ya Koji Miyoshi kutolewa kwa kadi nyekundu. Lakini, hilo halikuwa tatizo kwani Ibrahima Sissoko aliwafungia bao la kuongoza kwenye dakika 23, kabla ya Union kusawazisha kupitia kwa Benedict Hollerbach muda mfupi baadaye.
Kwa kuwa pungufu uwanjani, Bochum ilionekana kucheza kwa akili ili ipate sare. Katika kipindi cha pili, kipa wao Patrick Drewes alionyeshwa kadi ya njano kwa kuchelewesha muda. Na wakati kipa huyo akijiandaa kupiga mpira wa golikiki, alipigwa na kiberiti cha gesi kichwani. Kipa Drewes alipoona hicho, alianguka na kujishika kichwa. Mashabiki wa timu ya nyumbani walichukizwa, wakiona Drewes amelikuza jambo hilo na kuzua taharuki wakati kipa anapatiwa matibabu.
Dakika nne baada ya tukio hilo, mwamuzi aliwaambia wachezaji wa Bochum waende vyumbani ili kuwa salama. Na dakika nne nyingine baadaye, Union nao walikwenda vyumbani. Dakika 16 baadaye, wachezaji hao walirudi uwanjani kuendelea na mechi.
Bochum walirudi, lakini kipa wao hakuweza kuendelea na mechi, wakati huo walimaliza kufanya sub zao zote, hivyo straika Philipp Hofmann akaenda golini.
Lakini, wakati mashabiki wakiwa hawajui kama Hofmann ana uwezo wa kudaka au la, timu hizo mbili zilionekana kukubaliana kwamba lisifungwe bao jingine, hivyo timu ilibaki ikipigiana pasi yenyewe tu kwenye eneo lao.
Mambo yalibaki kuwa hivyo hadi mwisho, ubao wa mabao ukisomeka 1-1.
Lakini, mabosi wa Bochum waliamua kukataa rufaa kutokana na mwamuzi kuamua kuendelea na mechi wakati kipa wao Drewes aliumizwa na mashabiki. Na mahakama ya soka ya huko Ujerumani ilikubaliana na mashtaka hayo ya Bochum na kuamua kuwapa ushindi wa mabao 2-0.
Mkuu wa mahakama hiyo, Stefan Oberholz alisema “hakuna chaguo jingine”. Union ina wiki moja ya kupinga adhabu hiyo kama inataka.