Duh! Havertz naye majeruhi
Muktasari:
- Arsenal kwa sasa ipo Dubai, wakienda kufanya mazoezi kwenye hali ya joto huko Mashariki ya Kati wakati wakijiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City.
DUBAI, UAE: ARSENAL majanga yanaendelea kuikumba timu yao baada ya straika wao Kai Havertz kuumia wakati wakiwa kwenye mazoezini huko Dubai.
Arsenal kwa sasa ipo Dubai, wakienda kufanya mazoezi kwenye hali ya joto huko Mashariki ya Kati wakati wakijiandaa na mchezo wao ujao wa Ligi Kuu England dhidi ya Leicester City.
Badala ya kambi hiyo ya mazoezi iwe na faida kubwa kwenye kikosi hicho cha kocha Mikel Arteta, badala yake wamekumbwa na tatizo la kuongezeka kwa wachezaji majeruhi katika kikosi chao.
Kwa mujibu wa Mail Online, Havertz alipata maumivu ya misuli ya paja mazoezini mapema wiki hii.
Licha ya kwamba hakuna vipimo vilivyofichua ukubwa wa tatizo lake, lakini kinachoonekana ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa staa huyo kukosa mechi ya wikiendi ijayo.
Havertz, 25, amekuwa na msimu mzuri kwenye klabu hiyo ya Emirates, amefunga mabao 15 na kuasisti mara tano katka michuano yote - ikiwa ni namba bora ukilinganisha na msimu uliopita, alifunga mabao 14 na kuasisti mara saba baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Chelsea.
Majeruhi ya Havertz yamekuja kipindi kibaya kwenye kikosi hicho cha Arsenal, ambayo kwa sasa kijasho kinawatoka kutokana na ufiti wa Gabriel Martinelli, ambaye aliumia kwenye mechi dhidi ya Newcastle.
"Ndiyo, Martinelli anahisi maumivu," alisema Mikel Arteta na kuongeza. "Nadhani ni maumivu ya misuli yamemfanya akose raha uwanjani, atapimwa kuona ukubwa wa tatizo lake."
Martinelli na Havartz sasa wataungana na Gabriel Jesus ambao wanaweza kukosa mechi hiyo ya wikiendi, huku Arsenal ikiendelea kumkosa Bukayo Saka, ambaye pia ni majeruhi.
Mabeki Ben White na Takehiro Tomiyasu nao wamekosekana uwanjani kwa muda mrefu na kuna wasiwasi mkubwa kuhusu staa wa Japan. Tomiyasu aliumia goti na madaktari wa Arsenal wanafikiria kumfanyia upasuaji.
Arsenal inahitaji matokeo ya ushindi dhidi ya Leicester City ili kupunguza pengo la pointi baina yao na vinara Liverpool ili zibaki kuwa tatu, huku ikitambua kwamba miamba hiyo ya Anfield inayonolewa na Arne Slot itasubiri kukipiga na mahasimu wao Everton kwenye kipute cha Merseyside derby, Jumatano.