Duh! Chelsea ina kikosi kizima wodini

LONDON, ENGLAND. KOCHA wa Chelsea, Mauricio Pochettino amepata pigo jingine kwenye kikosi chake baada ya Enzo Fernandez na Axel Disasi kuumia na kuwa na hatihati ya kuwamo uwanjani kwenye mchezo wa kesho Jumatatu dhidi ya Everton.

Wachezaji hao walihitaji kufanyiwa uchanguzi wa kina kama watakuwa fiti kucheza mchezo huo wa kesho wa EPL Stamford Bridge.

Pochettino hakutaka kuelezea sana ukubwa wa majeruhi hao kwenye kikosi chake, hata hivyo haionyeshi kama ni ishu kubwa sana na huenda akawapanga hivyo hivyo kwenye kipute hicho.

Alisema: “Ngoja tuone. Wanafanyiwa tathmini. Wana shida tofauti na tunachoamini si tatizo kubwa sana, lakini tunasubiri kuona kama watakuwapo kwa ajili ya mechi. Walishindwa kufanya mazoezi baada ya mechi na Sheffield United.”

Kikosi hicho kina mastaa kibao ambao ni wagonjwa akiwamo Ben Chilwell, Levi Colwill, Wesley Fofana, Reece James, Romeo Lavia, Christopher Nkunku na Lesley Ugochukwu.

Wakati huo huo, Robert Sanchez na Raheem Sterling wanatazamiwa kukosa mechi hiyo ya kesho kwa kuumwa. Kabla ya mechi za jana, Chelsea ilikuwa inashika nafasi ya tisa EPL.