DR Congo v Jamaica kufuzu Kombe la Dunia kinawaka leo
Muktasari:
- Mechi nyingine itakuwa kati ya Iraq dhidi ya Bolivia, washindi wa mechi hizo watajikatia tiketi na kukamilisha jumla ya timu 45 tayari kwa fainali za Kombe la Dunia ambazo zifanyika kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Marekani, Canada na Mexico.
ZENICA, BOSNIA: HEKAHEKA za kuwania nafasi sita za mchujo kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia 2026 zinaendelea tena leo, Jumanne kwa timu nane za taifa Ulaya, ikiwemo Italia kupigania nafasi nne huku wawakilishi pekee kutoka Afrika, DR Congo wao wakikipiga usiku wa kuamkia kesho, Jumatano dhidi ya Jamaica.
Unaweza kusema kwamba leo na kesho ni siku za hesabu, siku ya kuamua hatma ya mataifa 12, Sweden ambayo imetoka kuichapa Ukraine kwa mabao 3-1 katika mechi ya nusu fainali ya mchujo itacheza dhidi ya Poland iliyoifunga Albania kwa mabao 2-1,takwimu zinaonyesha katika mechi tano zilizopita kati yao, Sweden imeshinda mechi nne huku ikipoteza moja dhidi ya Poland.
Mechi nyingine ya kusisimua kwa Ulaya itakuwa kati ya Kosovo dhidi ya Uturuki, hii inatazamwa kuwa huenda ikawa mechi ya upande mmoja kutokana na rekodi nzuri iliyonayo Uturuki kwa kushinda mechi zote tatu ambazo timu hizo zimewahi kukutaka katika mashindano yote.
Lakini pamoja na hilo, Kosova kwa sasa inaonekana kuimarika na ndio maana haijapoteza katika mechezo yake mitano iliyopita ikiwemo mechi ya nusu fainali katika mchujo, iliichapa Slovakia kwa mabao 4-3.
Jamhuri ya Czech yenyewe itakuwa na kibarua kizito cha kukabiliana na Denmark ambayo haijapoteza mechi saba za mwisho dhidi yao, hivyo itakuwa na kazi kubwa na ngumu ya kuvunja mwiko kutokana na kufungwa mechi tano na kuambulia sare katika mechi mbili.
Macho ya wengi katika mechi za Ulaya, yatakuwa kwa mabingwa wa Kombe la Dunia wa mwaka 2006, Italia ikiwa chini ya Gennaro Gattuso ambapo wakati huo alikuwa sehemu ya kikosi hicho, watakuwa na kazi ya kufanya dhidi ya Bosnia & Herzegovina ambayo inapambania kushiriki kwa mara ya pili michuano hiyo, mara yao ya kwanza ilikuwa 2014.
Mfungaji bora wa muda wote wa Bosnia & Herzegovina, Edin Dzeko ni kati ya wachezaji wa kutazamwa alifunga bao muhimu katika mechi iliyopita ya mchujo dhidi ya Wales (1-1), ambalo lilikuwa bao lake la nane mfululizo kimataifa.
Shujaa wa Italia katika mechi iliyopita ya mchuajo dhidi ya Ireland Kaskazini alikuwa Sandro Tonali, aliyefunga na kutoa pasi ya bao, wakati vijana hao wa Gattusso wakitinga fainali ya mchujo, hivyo anaweza kuendelea kuwa mmoja wa wachezaji muhimu katika mchezo wa leo.
Usiku wa kumakia kesho, matumaini ya Wakongomani na Waafrika kwa ujumla yatakuwa kwa DR Congo ambao watashuka dimbani huko Mexico kucheza dhidi ya Jamaica, hii itakuwa mara ya kwanza kwa timu hizi kukutana.
Mechi nyingine itakuwa kati ya Iraq dhidi ya Bolivia, washindi wa mechi hizo watajikatia tiketi na kukamilisha jumla ya timu 45 tayari kwa fainali za Kombe la Dunia ambazo zifanyika kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Marekani, Canada na Mexico.