Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sintofahamu Kombe la Dunia 2026 likikaribia

DUNIA Pict

Muktasari:

  • Tayari kumekuwapo na malalamiko kuhusu gharama kubwa za tiketi, mazingira ya viwanja, hali ya hewa na wasiwasi wa kukamatwa kwa watu kutoka mataifa mengine na kikosi maalumu nchini Marekani cha kupambana na wahamiaji haramu (ICE).

WASHINGTON, MAREKANI: KOMBE la Dunia limekuwa likitajwa kama tukio linalounganisha dunia kupitia mchezo wa mpira wa miguu, lakini zikiwa zimebaki takribani siku 70 na ushei kabla ya kuanza kwa mashindano hayo picha ya umoja imeanza kufunikwa na changamoto mbalimbali za kisiasa, kiusalama na kijamii.

Tayari kumekuwapo na malalamiko kuhusu gharama kubwa za tiketi, mazingira ya viwanja, hali ya hewa na wasiwasi wa kukamatwa kwa watu kutoka mataifa mengine na kikosi maalumu nchini Marekani cha kupambana na wahamiaji haramu (ICE).

Tunakuwekea changamoto sita zinazotishia ubora wa mashindano ya Kombe la Dunia mwaka huu katika nchi za Marekani, Mexico na Canada yanayotarajiwa kuanzia Juni 11 hadi Julai 19, mwaka huu.

DUNI 06

VIZUIZI VYA USAFIRI

Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino alisisitiza mwaka jana kuwa, “dunia inakaribishwa Marekani.

“Tutauza tiketi kati ya milioni sita hadi saba kwa mechi, na tutakuwa na watu kati ya milioni tano hadi 10 kutoka kote duniani wakija kufurahia Kombe la Dunia.”

Hata hivyo, kwa sasa hali inaonekana kuwa tofauti, kwani watu wengi wanaonekana kuwa na wakati mgumu kwenda Marekani kutokana na masharti yaliyowekwa na Marekani.

Sera ya “America First” chini ya Rais Donald Trump imesababisha kuwepo kwa vizuizi vya usafiri kwa nchi mbalimbali duniani, ikidaiwa kuwa ni juhudi za kudhibiti uhamiaji haramu.

Kutokana na hilo, viza za utalii zimekuwa ngumu zaidi kupatikana kwa mashabiki kutoka nchi kama Senegal na Ivory Coast, huku mashabiki wa Iran na Haiti wakikabiliwa na uwezekano wa kushindwa kabisa kuingia Marekani.

Zaidi ya hapo, mpango unaoitwa “Visa Bond Pilot Program” umeongeza ugumu zaidi, kwani unawalazimisha raia wa nchi kama Senegal, Ivory Coast, Algeria, Tunisia na Cape Verde zilifuzu kulipa hadi dola 15,000 kama dhamana ili kuruhusiwa kusafiri kwenda Marekani.

Hali hii imezua wasiwasi mkubwa kuhusu uwezekano wa mashabiki kusafiri kwenda Marekani ambako zaidi ya mechi 60 za michuano hiyo zitachezwa.

DUNI 03

BEI ZA TIKETI

Kumekuwa pia na malalamiko ya bei za tiketi. FIFA ilitoa idadi ndogo ya tiketi za dola 60 kwa mashabiki wa 48 zilizofuzu.

Hata hivyo, shirikisho la mashabiki barani Ulaya (Football Supporters Europe - FSE) lilipinga mara moja hatua hiyo likisema kuwa shirikisho hilo limefanya makosa makubwa katika uuzaji wa tiketi.

FSE ilisema kwamba imewasilisha malalamiko yao kwenda tume ya Ulaya ikidai kuwa kuna udanganyifu mkubwa umefanyika katika kutangaza bei za tiketi.

Inaelezwa tiketi za dola 60 zilishauzwa kabla hata ya kutangazwa rasmi, na zilizobakia ni zile za bei ghali ambazo asilimia kubwa ya mashabiki ni ngumu kuzinunua.

Mashindano ya mwaka huu yanadaiwa kuwa na bei kubwa mara saba ya ile ambayo ilikuwa katika mashindano ya Kombe la Dunia la mwaka 2022 huko Qatar.

DUNI 05

MAZINGIRA

Katika mashindano ya Kombe la Dunia la klabu mwaka jana, makocha na wachezaji kadhaa hawakuridhishwa na hali ya ubora wa viwanja, jambo ambalo linaonekana kuwa linaweza kutokea tena.

Kiungo wa Real Madrid na England, Jude Bellingham, alisema viwanja havikuwa vizuri kabisa. Kocha wa Paris Saint-Germain, Luis Enrique, alionyesha kutoridhishwa zaidi na uwanja wa Lumen Field uliopo Seattle, ambao utatumika katika mashindano ya mwaka huu.

“Kuna mashimo kila mahali, mpira ulikuwa unadunda kama sungura,” alisema Enrique kwa hasira baada ya timu yake kushinda mabao 2-0 dhidi ya Seattle Sounders.

Mbali ya ubora wa viwanja, pia kulikuwa na shida ya hali ya hewa. Mapumziko ya kunywa maji yalikuwa ya lazima kutokana na joto kali linaloikumba Marekani, huku kocha wa Chelsea, Enzo Maresca, akisema joto hilo lilikuwa kali kiasi cha kufanya iwe haiwezekani kufanya mazoezi ya kawaida.

Kiungo wa Chelsea, Enzo Fernandez, naye alikiri kuwa alihisi kizunguzungu wakati wa mechi.

Kutokana na hilo, FIFA imetangaza kwamba kutakuwa na utaratibu wa mapumziko ya dakika tatu ya kunywa maji katikati ya kipindi cha kwanza na cha pili katika kila mechi ya Kombe la Dunia la mwaka huu.

Hatua hiyo imepokelewa vizuri na baadhi ya watu, lakini wengine wameikosoa wakisema ni njia ya kimkakati ya kugawanya mechi katika vipindi vinavyofanana na mfumo wa Marekani, ili kuwapa wamiliki wa haki za matangazo fursa zaidi za matangazo ya kibiashara yenye faida.

Vilevile, kuna insha ya radi ambapo husababisha mechi kusimamishwa kwa muda mrefu kutokana na sheria za Marekani ambazo zinaeleza kwamba radi zinapopiga umbali wa maili 10 ni sharti mechi isimamishwe hadi hali itakapokuwa sawa.

“Kwangu mimi, huu si mpira wa miguu,” alisema Maresca alipokuwa kocha wa Chelsea baada ya mechi yao ya hatua ya 16 bora dhidi ya Benfica kusimamishwa kwa dakika 113. “Nadhani ni mzaha. Naelewa ni kwa sababu za usalama, lakini kama unasimamisha mechi saba au nane, ina maana pengine si mahali sahihi kufanyia mashindano haya.”

DUNI 01

KIKOSI CHA ICE

Jambo linalotia wasiwasi zaidi ni mazingira ya sasa ya kisiasa nchini Marekani. Jitihada za utawala wa Donald Trump za kukabiliana na uhamiaji haramu zimezua mabishano makubwa kote nchini humo, na katika video mbalimbali wananchi wameonekana wakiandamana kupinga kikosi maalum kinachokamata wahamiaji haramu nchini humo.

Mnamo Januari mwaka huu, watu sita walifariki wakiwa chini ya ulinzi wa ICE (Luis Gustavo Nunez Caceres, Luis Beltran Yanez Cruz, Parady La, Heber Sanchez Dominguez na Victor Manuel Diaz), huku wengine wawili (Renee Nicole Good na Alex Pretti) wakipigwa risasi na maafisa wa ICE jijini Minneapolis, tukio lililochochea maandamano makubwa.

Wasiwasi umezidi kuongezeka baada ya kaimu mkurugenzi wa ICE, Todd Lyons, kusema kuwa taasisi yake itakuwa sehemu muhimu ya mfumo mzima wa usalama kwa Kombe la Dunia.

“Tutajitoa kuhakikisha usalama wa mashindano hayo na kulinda washiriki wote na wageni,” alisema Lyons.

Kwa upande mwingine, mbunge kutoka New Jersey, Nellie Pou, aliwasilisha muswada uitwao ‘Save the World Cup’ unaolenga kuzuia ICE kufanya msako ndani ya umbali wa maili moja kutoka viwanja vya mechi au maeneo ya mashabiki wakati wa Kombe la Dunia.

“Kombe la Dunia linapaswa kuleta watu pamoja, si kuacha familia zikiishi kwa hofu kwamba maafisa wa ICE watakuwa nje ya viwanja,” alisema Pou siku ya Alhamisi, Machi 19.

DUNI 04

MAGENGE YA DAWA ZA KULEVYA

Masuala ya usalama pia yamezua mjadala mkubwa tangu mwezi uliopita kutokana na kuzuka kwa vurugu na mauaji huko Mexico, ambapo wanachama wa genge la dawa za kulevya la Jalisco New Generation Cartel walihusika katika mapambano makali ya risasi na jeshi la nchi hiyo baada ya kuuawa kwa kiongozi wao, Nemesio Oseguera Cervantes, wakati wa operesheni ya kijeshi.

Oseguera Cervantes, maarufu kama “El Mencho”, alikuwa mtu anayetafutwa zaidi nchini humo, na kuuwawa kwake kulisababisha takribani wanajeshi na askari polisi 26 kuuwawa ndani ya saa 24 tu baada ya kifo chake Februari 22.

Mexico inatarajiwa kuandaa mechi 13 za mashindano haya, zikiwemo nne katika mji wa Guadalajara, ambao upo katika jimbo la Jalisco, kunakodaiwa kuwa hali ya amani bado haipo sawa.

Hata hivyo, rais wa nchi hiyo, Claudia Sheinbaum alisisitiza kuwa vurugu zinazoendelea “hazina hatari yoyote” kwa mashabiki, na akaongeza kwamba ana mpango wa kupeleka askari wa usalama 100,000, wakiwemo wanajeshi 20,000 na maofisa wa polisi 55,000 kwa ajili ya kulinda wageni wataoingia nchini humo kwa ajili ya kushuhudia michuano hiyo.

DUNI 02

MAREKANI VS IRAN

Desemba iliyopita, Gianni Infantino alimkabidhi Donald Trump tuzo ya ‘FIFA Peace Prize’.

Hata hivyo, rais huyo wa Marekani sasa yupo katika mgogoro wa vita dhidi ya Iran, ikishirikiana na Israel katika kufanya mashambulizi.

Inaelezwa mgogoro huo umefanya mashabiki kusafiri kwenda Kombe la Dunia kuwa ngumu kutokana na mfumuko wa bei uliosababishwa na kufungwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz ambao ni maalum kwa ajili ya kupitisha meli nyingi za mafuta, hivyo kufungwa kwake kumesababisha mfumuko wa bei za usafiri.

Vita hiyo pia imesababisha Iran kueleza kuwa haitoshiriki Kombe la Dunia.

Iran imepangwa kucheza mechi zake zote tatu za hatua ya makundi nchini Marekani, na ombi lao la kuhamisha mechi hizo kwenda Mexico tayari limekataliwa na FIFA, huku Infantino akisisitiza kuwa Trump alimwahidi binafsi kwamba timu ya taifa ya Iran haitakuwa na shida yoyote katika ardhi ya Marekani. Hata hivyo, Trump bado hajabadilisha msimamo wake wa awali kwamba, “hajali iwapo Iran itashiriki au la, na hata ametamka hadharani kuwa hawezi kuhakikisha usalama wa timu ya taifa ya Iran.”