Dortmund yaiadhibu Copenhagen kwao
Muktasari:
- Bellingham amekuwa akipata dakika chache za kucheza kwenye Bundesliga tangu alipohamia Dortmund kwa pauni milioni 27 akitokea Sunderland majira ya kiangazi, lakini alitumia vizuri nafasi yake katika mechi yake ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutoa pasi ya bao.
COPENHAGEN, DENMARK: Jobe Bellingham ametoa mchango wake wa kwanza tangu ajiunge na Borussia Dortmund baada ya kusaidia bao la ufunguzi la Felix Nmecha, ambaye alifunga mara mbili na kuisaidia klabu hiyo ya Ujerumani kushinda 2-4 ugenini dhidi ya Copenhagen kwenye Uwanja w Parken, Denmark usiku wa Oktoba 21, 2025.
Bellingham amekuwa akipata dakika chache za kucheza kwenye Bundesliga tangu alipohamia Dortmund kwa pauni milioni 27 akitokea Sunderland majira ya kiangazi, lakini alitumia vizuri nafasi yake katika mechi yake ya pili mfululizo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa kutoa pasi ya bao.
Mshambuliaji Mjerumani, Nmecha alipokea pasi safi kutoka kwa Bellingham dakika ya 20 na kupiga shuti kali kutoka pembezoni mwa eneo la hatari lililojaa nguvu na usahihi.
Copenhagen ilisawazisha katika mazingira ya kuchekesha kwani mlinda mlango Gregor Kobel aliokoa shuti la chini kufuatia kona, lakini jitihada za Ramy Bensebaini za kuondoa hatari, mpira ulimgonga beki mwenzake Waldemar Anton na kuingia wavuni.
Bensebaini alijirekebisha dakika ya 61 kwa utulivu mkubwa alipofunga penalti baada ya Serhou Guirassy kuchezewa vibaya ndani ya eneo la hatari.
Nmecha aliongeza bao la tatu dakika ya 76 baada ya shuti lake kuguswa na beki na kumfanya kipa wa Copenhagen, Dominik Kotarski, ashindwe kuelekea upande sahihi.
Bellingham alionekana kuwa na hamu kubwa ya kufunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo, lakini ni Fabio Silva, aliyewahi kuchezea Wolves, aliyeongeza bao la nne mwishoni mwa mechi.
Viktor Dadason alipunguza tofauti kwa bao la kufutia machozi dakika za lala salama baada ya mpira wake wa kichwa kuvuka mstari.
Dortmund sasa itasafiri kuifuata Manchester City Novemba 5, 2025 ikiwa na pointi saba baada ya mechi tatu, huku Copenhagen ikibaki bila ushindi baada ya sare na Bayer Leverkusen na kupoteza 2-0 dhidi ya Qarabag.