Diogo Dalot afichua kinachoikwamisha Man United
Muktasari:
- Dalot aliifungia Man United bao la kuongoza dakika ya 58, kabla ya West Ham United kupata bao la kusawazisha kupitia kiungo wa Ufaransa, Soungoutou Magassa dakika ya 83.
Beki wa pembeni wa Man United, Diogo Dalot ameonyesha kukerwa na kitendo cha timu hiyo kushindwa kulinda bao la kuongoza walilolipata dhidi ya West Ham United, iliyolazimisha sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Old Trafford jana Alhamisi, Desemba 4, 2025.
Dalot aliifungia Man United bao la kuongoza dakika ya 58, kabla ya West Ham United kupata bao la kusawazisha kupitia kiungo wa Ufaransa, Soungoutou Magassa dakika ya 83.
Beki huyo anaamini Man United ilikuwa na presha mara tu ilipopata bao la kuongoza dhidi ya West Ham, na amesisitiza timu haiwezi kuendelea kupoteza pointi wakati ipo mbele kwenye uwanja wa Old Trafford.
Baada ya mechi hiyo, Dalot hakuweza kuficha hasira zake alipozungumza na Sky Sports, akilalamikia kushindwa kwa timu kuendelea kucheza kiwango kilekile baada ya kupata bao la kwanza.
“Tumekasirika. Tunahitaji kudhibiti mchezo zaidi, hasa hapa Old Trafford. Hatuwezi kuwa na wasiwasi kama tulivyokuwa baada ya bao. Labda tulikuwa wazembe zaidi kwenye umiliki wa mpira, kwa hiyo bila shaka tumekatishwa tamaa na sare hii. Mchezo ulikuwa mkononi mwetu,” amesema.
Alipoulizwa kwa nini Man United inashindwa kupata matokeo ya kuridhisha msimu huu, Dalot amejibu: “Hilo ndilo suluhisho tunalohitaji kulipata. Inaweza kusababishwa na vitu vingi. Haipaswi kuwa hivi kwa sababu tunapambana kwa dakika 60 kupata bao, na linapotokea tunapaswa kuendelea kufanya yale yale, hata kuongeza umakini, umiliki wa mpira ili tuwe na utawala zaidi. Hasa tunapopoteza mpira, lazima tuwe katika nafasi nzuri za kuurudisha.
“Kuhusu lile bao tulilofungwa mpira ulienda kwenye kona na tukaruhusu, ndio mambo tunapaswa kuyaepuka, hasa dhidi ya timu zinazocheza vizuri kwa kushambulia kwa kasi kama tulivyofahamu. Kwa bahati mbaya hatukuweza kumaliza mchezo lakini tunahitaji kujilaumu sisi wenyewe. Ni kosa letu zaidi na ninaipongeza West Ham.
“Matokeo ya aina hii yanakupa jambo la kufikiria. Hatuwezi kuwa tunaongoza uwanjani kwetu na kubaki dakika 30, halafu tusishinde mchezo.”
Manchester United, ambayo ilikuwa ikitafuta ushindi ili kusogea nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi ya EPL, sasa ipo nafasi ya nane ikiwa na alama 22, jambo linaloonyesha kuwa wamepoteza fursa ya kusogea karibu na nafasi za Ligi ya Mabingwa.
Kwa upande wa West Ham United imefaidika kidogo kutokana na sare hiyo, ikiwa imeongeza pointi moja na kuendelea kushikilia nafasi ya 18 katika msimamo, ikiwa na alama 12.