Wafanyakazi Man United ni kicheko tu
Muktasari:
- Uamuzi wa kurejesha hafla hiyo umefikiwa na viongozi wa timu hiyo baada ya mwaka jana tajiri Ratcliffe kuifuta.
MANCHESTER, ENGLAND: WAFANYAKAZI wa Manchester United watasherehekea msimu wa sikukuu kwa kufanya sherehe ya Krismasi pamoja kwa mara ya kwanza tangu ujio wa Sir Jim Ratcliffe.
Uamuzi wa kurejesha hafla hiyo umefikiwa na viongozi wa timu hiyo baada ya mwaka jana tajiri Ratcliffe kuifuta.
Gazeti la Daily Mail limeandika kuwa Omar Berrada, Afisa Mtendaji Mkuu mpya aliyejiunga na mashetani wekundu kutoka Manchester City, ndiye aliyesimamia mchakato mzima kuhakikisha suala hilo linafanikiwa.
Ratcliffe na viongozi wakuu wa Man United walikosolewa sana mwaka jana baada ya kufuta sherehe hiyo ikiwa ni sehemu ya mchakato wa Ratcliffe kubana matumizi.
Inaelezwa kuwa uamuzi mgumu wa kufuta hafla ya mwaka jana uliokoa zaidi ya pauni 100,000, huku bonasi ya kila mwaka pia ikipunguzwa kutoka pauni 100 hadi pauni 40.
Man United itafanya sherehe hiyo kwenye ukumbi wa ndani ya Old Trafford mwaka huu, tofauti na zamani ambapo ilikuwa ikifanyika kwenye hema nje ya uwanja, au Lancashire County Cricket Club na Victoria Warehouse.
Katika kikosi hicho kumekuwa na matukio kadhaa ya kupunguzwa kwa wafanyakazi ikiwa ni mwendelezo wa kubana matumizi.
Pia imeondoa huduma ya chakula cha mchana kwa wafanyakazi katika uwanja wa mazoezi na tajiri Ratcliffe ametetea uamuzi huo akisema anafanya hivyo ili kuhakikisha timu inapata faida na anaamini baada ya miaka mitatu, Man United itakuwa timu yenye kuingiza faida zaidi kubwa.
"Na itakuwa katika hali tofauti kabisa. Lakini lazima tupitie mabadiliko na kiasili hakuna anayependa mabadiliko."