Dili za kuibua vita dirisha la Januari 2026
Muktasari:
- Usajili huo wa katikati ya msimu unatoa fursa kwa klabu kuboresha vikosi vyao kwenye maeneo yenye shida ili kuwa vizuri. Timu zinaweza kufanya usajili wa kupanua vikosi vyao ua kuongeza nguvu ili kumaliza msimu vizuri.
LONDON, ENGLAND: DIRISHA la usajili wa mastaa wa soka la Januari limebakiza siku chache tu kufunguliwa ili kuzipa nafasi klabu za Ligi Kuu England kuboresha vikosi vyao kwa ajili ya kumaliza msimu kwa kishindo.
Usajili huo wa katikati ya msimu unatoa fursa kwa klabu kuboresha vikosi vyao kwenye maeneo yenye shida ili kuwa vizuri. Timu zinaweza kufanya usajili wa kupanua vikosi vyao ua kuongeza nguvu ili kumaliza msimu vizuri.
Timu zitaingia sokoni kufanya usajili kulingana na kitu inachotaka kukifanya katika kuelekea mwisho wa msimu na kuna timu zinazotaka ubingwa, kuna zinazopambana kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Ulaya na zile zilizopo kwenye vita ya kuepuka balaa la kushuka daraja. Kutokana na hilo, Januari hii itakuwa bize sana kwa klabu za Ligi Kuu England.
Hizi hapa dili za kibabe kabisa zinazoweza kutokea kwenye dirisha hilo la uhamisho wa Januari.
Elliot Anderson kwenda Man United
Manchester United inapambana kuimarisha safu yao ya kiungo ili kuwa na kikosi kitakachopambana kwenye Ligi Kuu England.
Kocha, Ruben Amorim bado hamwamini Kobbie Mainoo na ndiyo maana anawapa nafasi Casemiro na Manuel Ugarte ya kuanza kwenye kikosi chake.
Lakini, staa wa Nottingham Forest, Elliot Anderson, 23, yupo kwenye mipango ya miamba hiyo ya Old Trafford na huenda ikapambana kupata saini yake dirisha la Januari litakapofunguliwa.
Adam Wharton kwenda Man United
Staa wa Crystal Palace, Adam Wharton ni chaguo jingine la Manchester United la mchezaji wa safu ya kiungo wanayepanga kumsajili dirisha la Januari.
Man United mpango wake ni kufanya maboresho kwenye safu ya kiungo na ndiyo maana inahusishwa na kali huyo wa zamani wa Blackburn Rovers.
Wharton, 21, amekuwa kivutio na kusakwa na timu kubwa kutokana na kile anachofanya kwenye Ligi Kuu England tangu aliponaswa akutokea Championship, Januari 2024.
Franculino Dju kwenda Liverpool
Liverpool inapambana kwa sasa kurudi kwenye viwango bora vya walau msimu uliopita wakati waliponyakua taji la Ligi Kuu England.
Kikosi hicho cha Kocha Arne Slot kimefanya usajili wa pesa nyingi, lakini mambo yameshindwa kwenda sawa.
Staa wao waliyemsajili kwa uhamisho ulioweka rekodi, Alexander Isak atakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na kuvunjika mfupa wa mguu na hilo ndilo linalofanya miamba hiyo ya Anfield kutaka kumsajili Franulino Dju ili kuziba pengo.
Antoine Semenyo kwenda Man City
Ni mmoja wa wanasoka wanaowindwa na klabu kibao za Ligi Kuu England kutokana na kufanya vizuri katika kikosi cha Bournemouth kuanzia msimu uliopita hadi huu.
Fowadi huyo tayari ameshafunga mabao manane katika mechi 16 alizocheza kwenye Ligi Kuu England alizochezea kikosi cha Bournemouth.
Semenyo kwenye mkataba wake kumewekwa kipengele kinachohitaji kulipwa Pauni 65 milioni ili kuvunja na kinaanza kufanya kazi Januari 1.
Kinachoelezwa, Semenyo amezikataa klabu kadhaa za Ligi Kuu England na kuchagua kwenda Manchester City.
Marc Guehi kwenda Liverpool
Liverpool inatazamiwa kurudi mezani kwa Marc Guehi wakati huu wakipambana kuboresha safu yake ya ulinzi.
Nahodha huyo wa Crystal Palace alikaribia kujiunga na Anfield dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi kabla ya dili hilo likikwama kwenye dakika za mwisho kabisa.
Guehi ataondoka bure Selhurst Park mwishoni mwa msimu huu, hivyo Palace inaweza kulazimika kumpiga bei kwenye dirisha la Januari ili kuambulia chochote kitu.
Brennan Johnson kwenda Crystal Palace
Crystal Palace inakabiliwa na balaa la kuwapoteza nyota wake wawili, Wharton na Guehi, hivyo inajiandaa na mpango wa kumchukua Brennan Johnson ili atue kwenye kikosi chao.
Tottenham ipo tayari kumuuza staa huyo wa zamani wa Forest dirisha la Januari na hapo ndipo Palace inapoibuka kuhitaji huduma yake.
Johnson amekuwa akivutia timu nyingi ikiwamo Aston Villa na West Ham zinazohitaji saini yake, lakini Palace inaweza kumnyakua.
Kobbie Mainoo kwenda Chelsea
Kobbie Mainoo amekuwa akihusishwa na mpango wa kuondoka Old Trafford dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Kiungo huyo amekuwa akikosa nafasi chini ya kocha Amorim, ambaye amekuwa akimpa nafasi Casemiro kuanza kwenye eneo hilo la kiungo.
Chelsea imekuwa ikihusishwa na Mainoo na huenda akatua kwa mkopo huko Stamford Bridge licha ya kocha wa Man United, Amorim kumwambia mchezaji huyo asahau kabisa suala la kuondoka Januari.
Ivan Toney kwenda Everton
Everton inapambana kuongeza makali kwenye safu yake ya ushambuliaji na kwenda hilo kwenye mpango wao kuna harakati za kusajili huduma ya mshambuliaji Ivan Toney.
Everton inahitaji huduma ya mshambuliaji huyo wa zamani wa Brentford.
Straika huyo wa England kwa sasa anakipiga Al-Ahli huko Saudi Arabia, ambako alifunga mabao 13 katika mechi 19 alizocheza msimu huu. Toney yupo tayari kurudi kwenye Ligi Kuu England.
Jorgen Strand Larsen kwenda West Ham
West Ham United imeripotiwa kuwa na mpango wa kuvamia kwenye klabu ya wapinzani wao wa kupambana kunusurika kushuka daraja ili kwenda kuchukua mchezaji kwenye dirisha la Januari.
Jorgen Strand Larsen amekuwa na kiwango bora msimu huu, akifunga mabao 14 kwenye ligi akiitumikia Wolves kwa mkopo baada ya kutokea Celta Vigo.
Kiwango chake kinaripotiwa kuwavutia Wolves na wanaweza kumsajili jumla kwa Pauni 25 milioni. Lakini, West Ham inataka kuingilia kati.
Savinho kwenda Tottenham
Tottenham Hotspur ilijaribu kumsajili Savinho dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi, lakini ofa yao ya Pauni 60 milioni ilikataliwa na Manchester City.
Mbrazili huyo amecheza mechi 13 tu kwenye ligi msimu huu na amekuwa na wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha miamba hiyo ya Etihad.
Spurs bado inahitaji huduma yake na huenda ikarudi Etihad kwenye diriha la Januari ilimchukua winga huyo wa Kibrazili endapo Brennan Johnson ataondoka.