Spurs kushusha vyuma vya maana
Muktasari:
- Inaelezwa kiasi hicho ni kwa ajili ya kumsajili winga wa kushoto na ilitamani kusajili Savinho dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini dili lilifeli.
LONDON, ENGLAND: MABOSI wa Tottenham wametenga Pauni 150 milioni kwa ajili ya usajili dirisha la majira ya baridi.
Inaelezwa kiasi hicho ni kwa ajili ya kumsajili winga wa kushoto na ilitamani kusajili Savinho dirisha lililopita la majira ya kiangazi lakini dili lilifeli.
Kwa sasa lengo lao lilikuwa ni kumsajili staa wa Bournemouth, Antoine Semenyo, lakini nyota huyo wa kimataifa wa Ghana inadaiwa ameshafanya uamuzi wa kujiunga na Manchester City, pia anawindwa na Liverpool na Manchester United.
Ikiwa Man City itamsajili Semenyo, hilo linaweza kufungua mlango kwa Tottenham kurejea tena kwa Savinho ingawa mashabiki wa Spurs hawaonekani kuhitaji kuwa na imani naye sana kwa sababu hapati nafasi ya kubwa ya kucheza.
Savinho, 21, amefunga bao moja tu la Ligi Kuu katika mechi 42 aliyocheza akiwa Man City, ikiwemo mechi 25 alizoanza akiwa kikosi cha kwanza. Vilevile katika michuano yote, amecheza mechi 69 na kufunga mabao matano.
Frank alilazimika kucheza mechi nyingi za msimu huu bila ya mshambuliaji wake namba moja Dominic Solanke baada ya jeraha lake la kifundo cha mguu kuwa kubwa zaidi ya ilivyotarajiwa awali. Mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England sasa amerejea mazoezini ingawa bado hajaanza kucheza.
Spurs imehusishwa kwa miezi kadhaa na mshambuliaji wa FC Porto na Hispania, Samu Aghehowa, 21, ambaye huenda akawagharimu takriban Pauni 50 milioni.
Matatizo ya mara kwa mara ya majeraha ya Destiny Udogie pia yanaifanya klabu hiyo kuweka kipaumbele katika kumsajili beki halisi wa kushoto.
Udogie tayari amekosa mechi 11 msimu huu na atakuwa nje hadi mwezi ujao kutokana na jeraha la misuli ya paja, ikiwa ni mara ya pili kuumia msimu huu na awali alikosa mechi mbili kutokana na majeraha ya goti.
Spurs pia inaweza kumsajili beki wa kati jambo litakalompa uhuru Micky van der Ven kucheza kushoto kama anavyofanya akiwa na timu ya taifa ya Uholanzi.